Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara ya siku sita mkoani Morogoro, akitoa maelekezo ya kujengwa hospitali ya rufaa na kufufuliwa viwanda.
Katika mkutano wa mwisho ndani ya mkoa huo uliofanyika Agosti 6, 2024 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Rais Samia amemuelekeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutafuta Sh5 bilioni ili kuanza ujenzi wa hospitali ya rufaa.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo kutokana na ombi la Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, aliyeeleza hospitali ya rufaa ya mkoa imezidiwa nguvu.
“Hospitali tuliyonayo imezidiwa nguvu, tunaomba tupate hospitali nyingine ambayo itawezesha kuwahudumia wananchi wa Morogoro na kutoka maeneo mengine ya jirani, kuipunguzia mzigo hospitali iliyopo,” amesema Abood.
Akizungumzia hilo, Rais Samia amekiri kuwa hospitali hiyo haina hadhi ya kuitwa hospitali ya rufaa, hivyo ni lazima Serikali iingilie kati na kujenga nyingine.
“Kwa kweli hospitali iliyopo haikidhi vigezo kuitwa hospitali ya rufaa kwa ulimwengu wa leo. Nimempa Waziri wa Afya atafute angalau bilioni tano (shilingi) za kuanzia tuanze ujenzi wa hospitali ya rufaa kwa kuanzia majengo yatakayotoa huduma za mama na mtoto kabla ya kwenda kwenye huduma nyingine,” amesema Rais Samia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye tovuti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ilianzishwa mwaka 1945 baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ambapo majengo yake yalitumiwa kama kambi.
Serikali chini ya uongozi wa hayati Mwalimu Julius Nyerere iliamua kuyafanya majengo hayo kuwa hospitali.
Mwaka 2010 iliyokuwa Hospitali ya Morogoro ikawa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ikipokea rufaa kutoka vituo vyote vya afya vya Serikali, mashirika ya kidini na binafsi katika mkoa huo.
Mbali na hilo, Rais Samia ameeleza mpango wa Serikali wa kuurudishia hadhi Mkoa wa Morogoro kwa kuvifufua viwanda vilivyokuwepo awali kwa kuanzia na kiwanda cha vipuri kilichopo Mang’ula.
“Wanaojua historia ya Morogoro wanaelewa nafasi ya viwanda. Tunataka kurejesha ile hadhi ya Morogoro ya viwanda, tunataka Morogoro ikashindane na Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam. Tayari nimeshampa maelekezo Waziri wa Viwanda, Dk Selemani Jafo kuhakikisha viwanda vilivyopo havifi na vilivyokufa vifufuliwe hata kama havitazalisha yale mazao ya awali basi vizalishe vitu vingine.
Amesema hatua hiyo inalenga kuzalisha ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa Mkoa wa Morogoro ambao kwa sasa una fursa nyingi za kiuchumi zinazopaswa kuchangamkiwa.
Katika hilo, Rais Samia amewataka viongozi wa mkoa huo kuacha kuvutana, badala yake kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani humo.
“Uwepo wa reli na umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unafanya mkoa huu kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji. Reli zote mbili ile ya MGR na SGR zote zinapita kwenye mkoa huu. Nasaha zangu kwenu acheni mivutano, tengeni maeneo ya uwekezaji ili wawekezaji wakifika wakute maeneo waweke fedha zao uwekezaji uendelee,” ameagiza Rais Samia.
“Kwenye elimu tumejenga Chuo cha Veta katika kila wilaya, lengo vijana wajifunze kulingana na amali zilizopo kwenye maeneo yao, sasa kwa kuwa tumeamua kuifufua sekta ya viwanda katika Mkoa wa Morogoro ni imani yangu kwamba vyuo hivi vitazalisha nguvu kazi itakayotumika kwenye hivyo viwanda. Wito wangu itumieni vyema fursa hii vijana wakasome,” amesema.
Rais Samia hakukubaliana na ombi la kuufanya mkoa huo kuwa jiji akieleza bado haujakidhi vigezo vya kufikia hatua hiyo.
Ombi hilo liliwasilishwa na mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoa huo, Dk Christine Ishengoma ambaye alieleza tayari mkoa huo una vigezo vyote vya kuufanya kuwa jiji.
Akijibu kuhusu hilo Rais Samia amesema, “Kwa vipimo tulivyoviweka bado Morogoro kuwa jiji, kuna kazi kubwa inatakiwa kuendelea kufanyika na Waziri wa Tamisemi atasema kazi gani ifanyike ili Morogoro iweze kuwa jiji kwa sasa bado, hivyo tumizeni wajibu wenu Serikali ije kutimiza wajibu wake.”
Awali akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha sigara cha Serengeti (Mkwawa leaf) aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kiwanda hicho kinapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi mazingira.
Amesema hayo baada ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye kiwanda hicho na moja lilionyesha miti ikiashiria ni mapori ya kuni.
“Nimeona katika maonyesho yenu kuna banda lina vimiti miti, lengo lilikuwa kuwarahisishia Watanzania hasa wanawake, kuwa mapori haya mnayopanda ya kuni, tupande kwa wingi.
“Hata hivyo, hivi sasa Watanzania tuna ajenda ya nishati safi ya kupikia, kuni bado siyo nishati safi, tunataka mpande misitu ile lakini tunaomba mtuunge mkono kwenye nishati safi ya kupikia,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia umuhimu wa kiwanda hicho, Rais Samia amesema, “Nimeambiwa kiwanda kina wafanyakazi si chini ya 7,000, hiki cha tumbaku na kile cha kutengeneza sigara kikikamilika kitakuwa na wafanyakazi 12,000,” amesema.
Rais Samia amesema awali kulikuwa na madaraja ya tumbaku na lile la mwisho halikununuliwa, lakini hivi sasa kiwanda hicho kinanunua kila kitu hivyo kumpa faida mkulima.
“Kuanzia jani la tumbaku hadi kiungio cha jani, hakuna kinachotupwa kila kitu kwenye zao la tumbaku ni mali, hii inamuongezea mkulima faida,” amesema.
Rais Samia amezungumzia mpango wa Serikali wa bima ya afya kwa wote, akiomba kiwanda hicho kuunga mkono juhudi hizo ili wale watakaomwa vifua waweze kupata matibabu.
“Nimeambiwa kiwanda kimepanua uzalishaji na usafirishaji wa mazao, asilimia tano tu ndiyo itakayovutwa hapa nchini na inayobaki itakwenda nje, hivyo ile tano itakayovutwa hapa itakuwa na athari kidogo. Tunatarajia kiwanda kitatuunga mkono kwenye mpango wa bima ya afya ili wale watakaokuja na vifua na kukohoa wapate matibabu,” amesema.
Awali, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kiwanda hicho kilikuwa kinazalisha tani 65,000 na sasa uzalishaji umeongezeka huku akieleza changamoto ya ‘makinikia’ ambayo amesema ilikuwa kwenye zao la tumbaku na si kwenye dhahabu pekee.
“Kwenye tumbaku hii makinikia ilikuwa wananunuzi wanaingia mkataba na wakulima wanampa mkulima mbegu na kutaka azalishe kilo 1,000 akizalisha kilo 1,200 wanaikataa, mkulima anabaki nayo hajui pa kuipeleka kisha kama soko ni Dola moja wanakwenda kumpa nusu yake,” amesema.
“Kati ya mwaka 2016/17 kiwanda kilifungwa, kina mwaka wa pili sasa tangu kimeanza oparesheni kikiwa kinazalisha tani 80,000 huku lengo likiwa kuzalisha tumbaku ya shambani tani laki mbili,” amesema.