Kwenye Ngao ya Jamii sapraizi inakuja, mtego uko hapa

SIMBA wameweka kitu na Yanga wakaweka kitu. Simba Day na Wiki ya Mwananchi zimepita. Kila shabiki sasa ni mchambuzi wa soka mitaani kutokana na kile alichokiona Kwa Mkapa.

Lakini kiufundi kwa jinsi vikosi vilivyooneka wikiendi katika matamasha hayo, mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Agosti 8 huenda ukawa na sapraizi nyingi.

Miguel Gamondi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba walipanga pangua vikosi hivyo na kuja na mtazamo tofauti kutoa nafasi kwa kila staa kuonyesha ubora wake mbele ya mashabiki lakini za ndani zinasema kwamba kila mmoja alikuwa akimsoma mwenzie kwa mchezo wa Alhamisi.

Hakuna aliyeonyesha uhalisia wake ndani ya dakika 90 na huenda stori ikawa tofauti kabisa keshokutwa kuanzia saa 1 usiku.

Fadlu alishinda mabao 2-0 dhidi ya APR yakifungwa na Debora Fernandes na Edwin Balua walioingia kipindi cha pili.

Huo ulikuwa ushindi wao wa nne. Kambini Misri dhidi ya Al-Adalah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia kwa mabao 2-1, Telecom FC kwa mabao 2-1 na El Qanah FC kwa mabao 3-0 zote ni timu za madaraja ya chini Misri.

Siku iliyofuata, Yanga ikawapiga Red Arrows ya Zambia mabao 2-1. Ulikuwa ushindi wa tatu kwa Wananchi katika michezo minne waliyocheza ya kirafiki kipindi cha maandalizi. Ikumbukwe kuwa walianza maandalizi yao kwa kupoteza katika Jimbo la Mpumalanga lililo mashariki mwa Afrika Kusini kwa mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’, wakashinda bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy.

Baada ya michezo hiyo miwili ya michuano ya Mpumalanga, Yanga ilienda Johannesburg kumalizia michezo yake ya kirafiki kwa kucheza dhidi ya Kaizer Chiefs ya kocha wao wa zamani, Nasreddine Nabi, waliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 na kutwaa Kombe la Toyota.

Kulingana na kile ambacho vikosi hivyo imeonyesha katika michezo yao ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, hiki ndicho kimeonekana katika michezo yao na taswira ya itakavyokuwa kuelekea Kariakoo Dabi Agosti 8, 2024 huku ikisubiriwa sapraizi ya maana.

Huenda Alhamisi tukashuhudia Dabi yenye kasi zaidi kulingana na namna ambavyo vikosi vya timu zote mbili vimekuwa vikicheza.

Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya APR, Fadlu ameonyesha kuwa ni kocha mwenye kupenda soka la kushambulia kwa kasi, kila ambapo wachezaji wake walipokuwa wakivuka nusu ya pili ya uwanja walikuwa wakisuka mashambulizi yao kwa haraka.

Uwepo wa wachezaji wenye kasi katika maeneo yake ya kati (kiungo) na pembeni kama vile, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Jean Charles Ahoua, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Débora Fernandes Mavambo na Awesu Awesu uliwafanya kufika kwa haraka kwa wapinzani wao.

Simba ina mabadiliko makubwa ya kiuchezaji hata wakati ikiwa haina mpira wamekuwa wepesi wa kuutafuta. Mabadiliko hayo ya kiuchezaji na kwa namna ambavyo Yanga nao wamekuwa na kasi kuanzia nyuma hadi eneo lake la mwisho la ushambuliaji ni wazi kwamba itakuwa mechi kali na yenye mvuto wa aina yake.

Miongoni mwa mambo ambayo yanampasua kichwa Fadlu ni pamoja na eneo lake la mwisho la ushumbuliaji na hilo limejidhihirisha katika michezo minne waliyocheza ya kirafiki.

Unaweza kuona katika mabao tisa waliyofunga Simba ni bao moja tu lililofungwa na mshambuliaji wa kati kiasili ambaye ni Steven Mukwala, wakati wakiwa Misri kwa maandalizi ya msimu ujao Fadlu alikiri kuwa na kazi ya kufanya juu ya eneo hilo.

Kuwa na wachezaji wa maeneo mengine wenye uwezo wa kufunga ni faida lakini kocha huyo kutoka Afrika Kusini anataka kuona washambuliaji wake wakiwa na wastani mzuri wa kutumia nafasi ambazo wamekuwa wakizitengeneza.

Akimzungumzia Mukwala ambaye alikuwa akicheza soka la kulipwa Ghana, kocha wa zamani wa Yanga na Azam FC, Hans van der Pluijm anaamini mshambuliaji huyo anaweza kuwa suluhisho ndani ya kikosi cha Simba.

“Nimemwona akicheza hapa Ghana, ni kati ya washambuliaji wazuri sana, unajua wapo wachezaji ambao wanaweza kuanza kuonyesha makali yao kwa haraka na wengine huhitaji muda, anaweza kuchanganya mbele ya safari, ni mshambuliaji mwenye nguvu, kasi na maarifa,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi anayeishi Ghana.

Bado Yanga imeonekana kuwa na shida katika ishu ya kuzuia mipira ya juu, mfano mzuri ni bao walilofungwa na Ricky Banda katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Banda alifunga kwa kichwa akiruka peke yake mbele ya Aziz Andabwile ambaye katika mchezo huo alitumika kama beki wa kati ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza huku akicheza sambamba na Dickson Job.

Akizungumzia hilo, kocha wa timu za vijana wa Azam FC, Mohammed Badru alisema: “Hili ni tatizo kwa timu nyingi za Tanzania, mwalimu (Gamondi) anatakiwa kulifanyia kazi.”

Katika maboresho ambayo Simba na Yanga imefanya katika dirisha hili la usajili, wapo wachezaji ambao tayari wameanza kuonyesha makali yao na huenda wakaongeza makali ya vikosi hivyo.

Beki wa kati Chamou Karaboue; viungo Joshua Mutale, Debora Mavambo, Jean Charles Ahoua, Augustine Okejepha na Awesu Awesu hao ni baadhi ya nyota wapya kwa Simba ambao wameanza kuonyesha makali yao katika michezo minne waliyocheza ya kirafiki.

Viwango vya wachezaji hao vimebeba matumani ya mashabiki wa Simba katika safari mpya ya ujenzi wa kikosi chao.

Tofauti na Simba, Yanga imefanya maingizo machache ambayo yanaonekana ni kama mwarobaini hasa katika maeneo ambayo walionekana kuwa na mapungufu msimu uliopita.

Usajili wa Prince Dube, Jean Baleke umeonekana kuwa na matumaini kwa Yanga katika safu yao ya ushambuliaji kutokana na walichokifanya washambuliaji hao katika michezo ya kirafiki.

Duke Abuya ameonyesha kuna kitu anaweza kukiongeza kwenye kikosi cha Yanga tofauti na Clatous Chama ambaye bado anajitafuta, eneo lingine ambalo Yanga imelifanyia maboresho ni beki ya kushoto na Chadrack Boka ameanza kuonyesha makali yake.

Ukiangalai vikosi vya timu zote mbili Simba na Yanga vilivyocheza katika mechi zao za matamasha, kulikuwa na namna ambayo makocha wao wameamua kuficha jambo.

Fadlu katika mchezo dhidi ya APR, alipanga kikosi ambacho golini alikuwepo Ally Salim, mabeki ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Chamou Karabou na Che Malone Fondoh. Katika viungo aliwapanga Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin, Awesu Awesu, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua, kisha mbele akasimama Steven Mukwala.

Hapa Faldu alianza na mfumo wa 4-5-1 wenye shepu ya diamond akiwatumia viungo wakabaji wawili kwa maana ya Ngoma na Mzamiru, kisha Mutale, Ahoua na Awesu wakiwa kwenye kiungo cha ushambuliaji, mbele akasimama Mukwala. Kule nyuma mabeki wakabaki wanne.

Ukiangalia Simba ilivyoanza na wachezaji walioingia kipindi cha pili, inatoa picha kwamba Fadlu ana kazi ya ziada ya kufanya kupata kikosi chake cha uhakika kwa sababu Debora Fernandes Mavambo na Augustine Okejepha waliokuja kuingia badala ya Ngoma na Mzamiru, walikiwasha sana na kusababisha kupatikana ushindi huo huku Mavambo akipachika bao la kwanza kabla ya Edwin Balua ambaye naye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awesu.

Kila mchezaji wa Simba aliyepewa nafasi alionekana kuwa na njaa ya mafanikio kitu ambacho kinabaki kwenye benchi la ufundi kukuna kichwa zaidi nani anapaswa kuanza na nani asubiri.

Gamondi na chama lake la Yanga ambalo halina mabadiliko makubwa ya kikosi kutokana na uwepo wa maingizo mapya saba, naye anaingia kwenye mtego wa jinsi ya kupanga kikosi chake.

Ukiangalia katika mchezo wa juzi dhidi ya Red Arrows ni kama alikuwa akifahamu kwamba Simba wanawafuatilia, hivyo akaamua kukivuruga kikosi chake kisitambulishe haraka kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Katika kikosi chake, golini alianza na Djigui Diarra, mabeki Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Dickson Job na Aziz Andabwile. Viungo wakasimama Khalid Aucho, Duke Abuya, Pacome Zouzoua na Clatous Chama, mbele wakasimamishwa Jean Baleke na Clement Mzize. Mfumo wa Gamondi ulikuwa ni 4-4-2, nyuma mabeki wanne na kati viungo wanne, mbele washambuliaji wawili.

Kipindi cha pili Gamondi akaamua kuwatoa wachezaji wote walioanza kikosi cha kwanza, wakaingia Khomeny Abubakari, Denis Nkane, Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Stephen Aziz Ki, Prince Dube na Kennedy Musonda.

Kama ilivyokuwa kwa Simba, Yanga nayo kipindi cha pili ilifunga mabao mawili kuptia wachezaji waliotokea benchi, Aziz Ki na Mudathir ambao nyota hawa msimu uliopita katika kikosi cha Gamondi ulikuwa huwakosi katika ile 11 ya kwanza.

Alichojaribu kukifanya Gamondi ni kuvuruga kikosi chake kisionekane wazi kwani hakumtumia kabisa Yao Kouassi ambaye ni panga pangua kikosi cha kwanza akicheza beki wa kulia, kumtia Kibwana kisha baadaye Nkane, ulikuwa mtego kwa wapinzani.

Andabwile naye kuchezeshwa beki wa kati sambamba na Job badala ya Bacca, kuna kitu Gamondi alijaribu kukificha Simba wasikione. Ile kombinesheni ya Pacome, Chama na Aziz Ki, pia haikuwepo kutokana na Aziz Ki kutokea benchi wenzake wakianza. Maxi naye alianzia nje wakati ni mchezaji ambaye Gamondi humwambii kitu kwenye kikosi chake cha kwanza.

Mbali na yote hayo, Gamondi naye ana kazi ya kufanya katika upangaji wa kikosi chake cha kwanza kwani eneo la kiungo ndiyo linaonekana kuwa na changamoto sana. Anaye Khalid Aucho, Jonas Mkude, Salum Abubakar, Aziz Andabwile na Mudathri Yahya ambao kiasili ni viungo wakabaji. Viungo washambuliaji wapo Clatous Chama, Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Shekhan Khamis, Denis Nkane, Farid Mussa na Duke Abuya.

Ikitokea siku amepanga kikosi cha mfumo wa 4-5-1, anapaswa kuchagua viungo watano pekee kati ya 13 alionao. Kati ya hao 13, mara kwa mara kikosini wasiokosekana ni Aucho, Mudathri, Aziz Ki, Pacome na Maxi Nzengeli, sasa wameongezeka Aziz Andabwile, Clatous Chama na Duke Abuya, ambao ukiangalia harakaharaka, wana nafasi zao kikosini, hivyo kazi ipo hapo. Usimsahau Mkude naye huwa anakichafua.

GAMONDI, FADLU WANASEMAJE?

Kuhusu kikosi chake, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema: “Nina furaha namna tulivyofanya pre-season na jinsi kazi ilivyokwenda, tulipambana kuhakikisha tunafanya vizuri, kama unavyofahamu mechi za pre-season siyo tu kuangalia matokeo bali ni namna gani wachezaji wanafuata yale yote ambayo tuliyojifunza.

“Pia imekuwa rahisi sana kwa wachezaji wapya kuingia kwenye falsafa tunayoitumia, kwa hakika imekuwa jambo nzuri na ninachukua nafasi hii kuwapongeza wote kwa kile walichokionyesha.”Kwa upande wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alisema: “Mapumziko nilikaa na wachezaji wangu kuwapa mbinu za kwenda kufanya baada ya kipindi cha kwanza kuonekana tukicheza taratibu mpira hauendi sana mbele, kipindi cha pili tuliwaweka wapinzani kwenye matatizo baada ya kuwapa presha, tukashinda.”

Related Posts