Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la kulawitiwa na kubakwa kwa msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Agosti 4, 2024 zilisambaa video katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana watano wakidaiwa kumbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimtuhumu kwa kile kilichosikika katika video hiyo kuwa ametembea na mume wa mtu.
“Jeshi la Polisi limekuwa likipokea simu nyingi kutoka kwa waandishi wa habari wakiuliza tumefikia hatua gani kwenye uchunguzi wa video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha tukio la binti aliyefanyiwa vitendo vya ukatili.
“Jeshi la Polisi lingependa kueleza kuwa, uchunguzi unaendelea vizuri na wananchi waendelee kuwa nasubira kwani taarifa itatolewa baada ya kukamilisha yale ambayo sheria za nchi zinavyoelekeza,” inaeleza taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.
Pia, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kutafakari namna inavyoendelea kujadili jambo hili na kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kama hakuendelei kumuumiza binti huyo na familia yake.
“Pia, tunaendelea kusisitiza mwenye taarifa ya ziada atuwasilishie kwa njia iliyosahihi kwa kutumia mifumo iliyoopo bila kuendelea kumuumiza,”inaeleza taarifa hiyo.
Mapema leo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema tayari vyombo vya dola vimeshawatia nguvuni watuhumiwa waliombaka na kumlawiti msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Masauni amethibitisha kutiwa nguvuni kwa vijana hao leo, Jumanne Agosti 6, 2024 alipotafutwa na Mwananchi Digital kwa njia ya WhatsApp.
Katika ujumbe mfupi aliotumiwa kuulizwa iwapo watuhumiwa hao wameshakamatwa, Masauni alijibu kwa kuandika “tayari” kupitia ujumbe huohuo wa njia ya WhatsApp.