Sauli kuzikwa kesho kijijini kwao Chunya

Mbeya. Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila unatarajiwa kuzikwa kesho Jumatano Agosti 7,  2024 katika Kijiji cha Godima wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya. 
Mwalabila  maarufu kwa jina la Sauli aliyefariki dunia Agosti 4,  2024 kwa ajali ya gari mkoani Pwani, mwili wake unatarajia kusafirishwa leo Jumanne Agosti 6, 2024 kwenda Mbeya.
Dada wa marehemu, Ericka Mwalabila ameiambia Mwananchi Digital kuwa kwa sasa wapo katika utaratibu wa usafirishaji wa mwili kwa ajili ya maziko.
Amesema mwili utasafirishwa kwa ndege kutoka mkoani Pwani alipopata ajali.
Sauli katika uhai wake, alikuwa mwekezaji kwenye sekta ya usafirishaji akimiliki mabasi yaendayo mikoani pamoja na migodi ya dhahabu Wilaya ya Chunya.
Keneth Jackson, mmoja wa wafanyakazi wake, akizungumza na Mwananchi Agosti 4, 2024 alisema Mwalabila alikuwa msimamizi mkuu wa migodi hiyo, hivyo wanasubiri uamuzi wa familia.

Related Posts