Dar es Salaam. Sekta ya uzalishaji viwandani, usafiri, ujenzi wa majengo ya biashara, utalii na kilimo zimetajwa kuongoza katika kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Tanzania kati ya mwaka 2021 hadi mwaka 2024.
Kupitia miradi hiyo jumla ya ajira 353,133 zimetengenezwa huku kilimo kikiongoza kwa kuzalisha kazi kwa watu.
Jambo hilo linamfanya mtaalamu wa uchumi kuishauri Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika maeneo mengine inayotamani mitaji hiyo ielekezwe huko.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne, Agosti 6, 2024 na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akifungua kongamano la uwekezaji katika sekta ya utalii jijini Dodoma kwenye Maonyesho ya Wakulima (Nanenane).
Profesa Mkumbo amesema kati ya miradi 1,484 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ndani ya kipindi hicho, 1,275 iligusa sekta tano pekee.
“Uzalishaji viwandani unaongoza kwa kuwa na miradi 608 sawa na asilimia 41, ukifuatiwa na usafiri na usafirishaji miradi 262, utalii miradi 142, majengo ya biashara miradi 140, kilimo 123,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema jumla ya ajira 353,133 zinazotarajiwa kuzalishwa kutokana na miradi ya uwekezaji huo na katika ajira hizo, asilimia 32.7 zilitokana na kilimo, ikifuatiwa na viwanda vinavyotoa asilimia 27 ya ajira, usafiri na usafirishaji asilimia 11.1, majengo ya biashara asilimia 3.2 na utalii asilimia 2.9.
Kufuatia suala hilo, Profesa Mkumbo amesema kama nchi inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya ufanyaji biashara, ukuaji wake na uwekezaji ni njia ya uhakika ya kuleta utajiri na kuondokana na umaskini katika nchi.
“Na hii ndiyo tofauti ya msingi kati ya nchi maskini na nchi tajiri duniani. Hatua moja kuelekea maendeleo ni kuweka mazingira mazuri kwa watu kufanya biashara,” amesema Profesa Mkumbo.
Katika maelezo yake, Profesa Kitila amesema:“Yeyote anayekwamisha biashara na uwekezaji ni mtu hatari kwa kuwa anakwamisha jitihada zetu za kujinasua katika umaskini.”
Ametumia nafasi hiyo kuwataka waliopewa dhamana katika utumishi wa umma kuona uwezeshaji biashara ni jukumu lao la msingi katika kusababisha biashara zinakue.
“Hiki kiwe ni moja ya vipimo muhimu vya ufanisi katika utendaji wetu. Tuone wakuu wetu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wakijivunia na kushindana kwa idadi ya biashara na uwekezaji waliosababisha kutokea na kukua katika maeneo yao ya kazi,” amesema Profesa Mkumbo.
Akieleza namna sehemu nyingine za uwekezaji zinavyoweza kuguswa kirahisi, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo ameshauri uboreshaji wa miundombinu ili kuvutia watu kuwekeza katika maeneo ambayo kama nchi inalenga kuyakuza.
“Kama unataka watu waende kwenye uvuvi unatengeneza miundombinu wezeshi ili akija aone anaweza kupata faida, wao hawapendi risk kwenye uwekezaji wao, ni kazi yako wewe kutengeneza mazingira ya biashara ili akiona miundomninu ajue anaweza kupata faida,” amesema Profesa Kinyondo.
Akitolea mfano wa uwekezaji uliofanywa Bandari ya Dar es Salaam amesema DP World ilikuwa ikifanya kazi katika maeneo mengine lakini ilikuja Tanzania baada ya maboresho kufanyika.