Mwanadada shabiki wa mpira na mwanamitindo, Subira Wahure maarufu kama Susu Kollexion, ambaye mara nyingi huwa anawashangaza watu baada ya kuonekana akiwa amevalia jezi za Simba na Yanga, amesema anaamini kwamba mashabiki wa Jangwani ni bahili kuliko wale wa Msimbazi.
Susu ameweka wazi kuwa hana timu ingawa alishiriki matukio yote ya siku za klabu hizo hivi karibuni, lakini mashabiki wa Simba sio bahili kama wa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa ofisini kwake Tabata, Dar es Salaam, alimesema, yeye sio mshabiki wa timu yoyote ila ni mpenzi tu wa soka la Tanzania, ndio maana anavalia jezi yoyote.
Aidha alisema, hapo awali alikuwa mshabiki lia lia wa Wekundu lakini baadae akaona asijipe mawazo, kwani mpira ni jambo la furaha na sio la presha.
“Sasa nimekuwa mshabiki wa timu zote ila kwa kuwa mimi ni Mwanamitindo siku huwa na shona nguo za rangi mbili nyekundu na kijani kila watani hawa wanapokutana na pindi nilipoanza kutangaza ndipo niligundua upande upi una mashabiki wa kishua,” amesema.
“Mashabiki wa Simba ndio wanaoongoza kununua pindi ninapokuwa na mashindano ya mavazi. Hii inaonyesha kuwa hawana ubahili kama wapinzani wao, hivyo naweza kusema ushabiki umenitengenezea soko kubwa la biashara.”
Watani hao wa jadi wanatarajiwa kukutana Alhamisi, Agosti 8, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii, huku Yanga ikiwa na rekodi ya kutolewa na Wekundu hao mwaka jana.