Kaimu Meneja Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Kutoka Dodoma jiji Mhandisi Kasongo Molijo akisikiliza wananchi Waliotembelea Banda la TARURA (hawapo pichani) katika Maonesho ya Kilimo Kitaifa Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Bi. Catherine Sungura akimuonesha Mwananchi jarida lenye taarifa za miradi ya barabara zilizojengwa wakati alipotembelea Banda la TARURA kwenye Maonesho ya Kilimo Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu Kaimu Meneja Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Kutoka Dodoma jiji Mhandisi Kasongo J. Molijo ameeleza changamoto wanayoipata Kutokana na wananchi kutupa taka hovyo kwenye mitaro na mitaro hiyo kuziba.
Akizungumza katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma amesema kuna baadhi ya watumiaji wa barabara hususani watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto wamekuwa wakitumia barabara vibaya.
“Sisi Kama TARURA tunapitia changamoto kubwa sana kutokana na wananchi kutupa taka kwenye mitaro na kusababisha mitaro hiyo kuziba na kupelekea maji ya mvua kutuama barabarani na kuleta uharibifu mkubwa katika barabara hizo.
Mhandisi Kasongo alisema kuwa TARURA inalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuzibua mitaro hiyo wakati fedha hizo zingeweza kupelekwa maeneo mengine kutatua changamoto za barabara kama watumiaji hao wangeepuka kutupa taka katika mitaro
Amesema kuwa TARURA inazidi kupambana na ujenzi wa barabara ambapo kuna miradi mingi inayoendelea sasa hivi ikiwemo miradi midogo ya matengenezo na miradi mikubwa ya barabara za lami, lengo ni kuhakikisha maeneo mengi katika Jiji la Dodoma yanafikika kirahisi.
“Tuna barabara ambayo inajengwa kutoka Kisima cha nyoka kwenda mpaka Nkuhungu ili kuhakikisha wananchi kutoka Nkuhungu wanafika mjini kiurahisi bila kuwa na kikwazo cha aina yoyote. ” Mhandisi Kasongo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Bi. Catherine Sungura amesema kuwa TARURA inawafahamisha wananchi na kuwapa elimu ya matumizi mazuri ya miundombinu ya barabara ikiwemo mifereji ya maji.
TARURA imeweza kuwasaidia wakinamama akitolea mfano wajawazito kutokana na kujenga barabara maeneo ya vijijini na kazi kubwa sana imefanyika hasa vijijini.