MWANASPOTI lilikuwepo kwenye Tamasha la Simba Day na kulikuwepo na mastaa wengi waliohudhuria shoo hiyo kali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na ilikuwa maalumu kwa utambulisho wa nyota mpya wa kikosi hicho pamoja na mtoko mpya (jezi) za msimu ujao 2024/25.
Katika pitapita zake, mara paap! uso kwa uso na msanii wa Bongo Fleva, Tunda Man ambaye ni shabiki lialia wa miamba hiyo ya soka nchini.
Kama kawaida Mwanaspoti likaomba Dakika 5 tu za kuteta naye kidogo na hasa kuhusu timu yake, usajili iliyoufanya na mchezo wa Dabi ya Kariakoo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kesho kwa Mkapa.
Tunda Man ameanza kwa kusema aliyoyaona kwenye kikosi hicho, huku akikiri kuvutiwa na usajili uliofanywa na kutamba hakuna timu ya kuizuia Simba kuchukua ubingwa wake msimu ujao.
“Katika vitu ninavyofurahia hapa duniani basi cha kwanza ni kusali ili kujiwekea mazingira mazuri nitakapochukuliwa, lakini cha pili ni kuifunga Yanga kila tunapocheza nao na hii Dabi watakula za uso mapema sana. Ni kitu kinachonipa furaha sana, nawaomba tu Yanga wasitokee uwanjani maana watapata aibu na kuweka historia mbaya,” amesema Tunda Man.
“Mimi naifuatilia kila siku klabu yangu na najisikia furaha sana kuwa shabiki wa simba. Sasa kwa usajili huu lazima tumfunge Yanga,” ameongeza.
Mwanaspoti: Kwa kuwaangalia nyota wa Simba kwenye mchezo wao uliopita, unawazungumziaje?
Tunda Man: Pamoja na kuchelewa kuingia uwanjani kutoka Mvomero, ila niliwahi kuiona timu yangu ikianza kucheza, ukweli timu iko vizuri, ina Morari ya ushindani, usajili wa wachezaji wapya na waliobaki inaonyesha timu itafikia malengo msimu ujao. Mchezaji kama, Debora Fernandes, Joshua Mutale, Valentino Mashaka, Edwin Barua, Ladaki Chasambi na wengine wengi watafanya poa.
Mwanaspoti: Unawaambiaje Yanga kuhusu mchezo huo wa Alhamisi?
Tunda Man: Kwa kifupi wakitaka kupunguza stresi na kuwa na maisha marefu duniani, shabiki wa Yanga Alhamisi kaa nyumbani, kwa sababu unaweza kupaona nyumbani kwako kutoka uwanjani ni kama unaenda mkoani, huo ndiyo ujumbe wangu. yaani Kwenda patakuwa karibu lakini kurudi patakuwa ni mbali sana kwa kipigo watakachopata Yanga.
Mwanaspoti: Utabiri wako ni nini wa matokeo ya mechi hiyo?
Tunda Man: Yaani Simba Alhamisi haiwezi kufungwa na Yanga, litakufa jitu siku hiyo kwa mabao matatu tu, yaani siku hiyo ni Ubaya Ubwela dakika ya themanini na sita goli tatu nyavuni zinakuwa zishawekwa na Simba.
Mwanaspoti: Unawaambia nini wachezaji wa Simba?
Tunda Man: Mwaka huu tunataka heshima, tunataka kuchukua ubingwa kuanzia shirikisho, ligi kuu na kuwa namba moja Afrika, hivyo tunawaomba wacheze mpira kwa kushirikiana, wapendane wasiwe wachoyo wa kupeana pasi uwanjani, wasomane mapema.
Mwanaspoti: Kitu gani kimekufurahisha Simba baada ya hizi heka heka za kukaribia kuanza ligi kuu?
Tunda Man: Kwanza kurudi kwa Mo Dewj, nimefurahi sana na niseme tu mwaka huu Simba hamtuambii kitu ila cha moto watakiona. Timu zingine zijipange kwenye Ligi na pili usajili una kiwango cha hali ya juu, kikubwa ni kuwapa muda wachezaji wetu, sio muda wa kuanza kuwalaumu kwa kuwaona tu mechi moja.
Mwanaspoti: Inasemekana una shida na viongozi wa Simba ndio maana hukupata nafasi ya kutumbuiza.
Tunda Man: Ukweli sina shida na uongozi wa Simba, mbona napewa nafasi mara nyingi tu kutumbuiza na kama kuna kiongozi ndani ya Simba nimemkwaza anisamehe, lakini mimi najua sina tatizo lolote na kiongozi yeyote, ila kwa hili la Simba Day ya juzi sababu ya kutotumbuiza ni kutokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Sababu nilipokea ujumbe kutoka kwa mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji akinitaka niwe sehemu ya wasanii siku ya Simba Day tena nitumie nafasi hii niwaombe msamaha viongozi wangu wa Simba, majukumu niliyokuwa nayo nje ya uwezo wangu nikashindwa kuwa sehemu ya wasanii walioimba katika tamasha, nilikuwa katika ziara Mvomero.
Mwanaspoti: Vipi habari za wewe zilisambaa kutaka kuhamia Yanga?
Tunda Man: Hivi hizi habari zinatoka wapi? Naona zilisambaa sana jamani. Mimi ni Simba na nitabaki kuwa Simba, hata waniue Simba sihami. Sasa niende Yanga kufanya nini jamani? mimi Simba ifanye vibaya au vizuri nitabakia kuwa Simba. Hapa tayari ni wimbo wa Tarehe 8 ukiacha huu wa Simba Day nilioutoa.