Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa uchunguzi wa kesi ya kuchepusha fedha na kuisababisha hasara ya Sh2.16 bilioni Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) unaendelea.
Kesi hiyo inamkabili mhasibu wa benki ya Habib African, Clement Kiondo (42) na wenzake tisa, wakiwemo wafanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wanaoshtakiwa kwa mashtaka 48, yakiwemo ya kughushi, kuchepusha fedha na kuisababishia hasara TGFA.
Wanaodiwa kughushi na kuwasilisha nyaraka za hundi na fedha wakionyesha Ofisi ya Waziri Mkuu imeridhia wapatiwe Kampuni ya Kalembo General Enterprise na Karimu G. Husein.
Wakili wa Serikali, Frank Rimoy leo Agosti 6, 2024 wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 26/2023 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya amedai bado wanaendelea na uchunguzi wa shauri hilo, hivyo ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 5, 2024 itakapotajwa. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Mbali na Kiondo, washtakiwa wengine ni Samwel Kyondo (52) na Fatuma Abdulaziz (52), ambao ni wafanyakazi wa Benki ya NBC.
Wengine ni Killian Kilindimo na wafanyakazi wa Benki ya Habib Africa ambao ni Devotha Masmini (52) na Catherine Mkelo (54).
Washtakiwa wengine ni Varelia Mhina (58), na Christopher Mduma (59) wote wafanyakazi wa Benki ya NBC. Mfanyabiashara Peter Tema (39) na wakili wa kujitegemea Henry Kishaluli.
Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu washtakiwa wote wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba mosi, 2011 na Machi 11, 2014 mkoani Dar es Salaam.
Inadaiwa katika kipindi hicho kwa kukusudia washtakiwa waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia Sh2.16 bilioni kwa njia ya ulaghai, mali ya TGFA.
Katika shtaka la kughushi na kuwasilisha nyaraka ya uongo, Clement na Kyondo wanadaiwa Juni 26, 2012 wilayani Ilala kwa nia ya kudanganya watengeneza nyaraka ya uongo ya malipo yenye thamani ya Sh542 milioni wakionyesha fedha hizo zimetolewa na TGFA na kisha kuwasilisha nyaraka hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu, eneo la Magogoni wakati wakijua ni uongo.
Clement, Kyondo, Abdulaziz na Masmini wanadaiwa Agosti 29, 2014, katika benki ya NBC tawi la Viwandani, kwa pamoja walighushi nyaraka ya fedha yenye thamani ya Sh98 milioni ikionyesha Ofisi ya Waziri Mkuu imeridhia fedha hizo ipewe Kampuni ya Kalembo Gereral Enterprises, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Kiondo na Masmini wanadaiwa Aprili 17, 2012 katika Benki ya Habib African walichepusha faida halali Sh59 milioni wakionyesha Ofisi ya Waziri Mkuu imeridhia kiasi hicho apewe Karim G Husein, wakati wakijua kuwa nyaraka walizowasilisha zilikuwa za kughushi.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Oktoba mosi, 2011 na Machi, 2014 jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu na vitendo vya uhalifu waliisababishia TGFA hasara ya Sh2.16 bilioni.