Wakimbizi wa Burundi washtukiwa kinachowafanya wasirejee kwao

Kasulu. Urejeaji wa hiari wa wakimbizi kutoka Burundi wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, umekumbwa na changamoto, huku wakimbizi hao wakisita kurudi kwao kwa sababu ya matumaini ya kupewa uraia wa Tanzania au kupelekwa katika nchi za Ulaya.

Haya yameelezwa leo Jumanne Agosti 6, 2024 na Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu, Siasa Menjenje baada ya Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kukutana na kuwahamasisha wakimbizi hao kurudi kwa hiyari kupitia kampeni ya “Njoo utuambie”.

Menjenje amesema kati ya Januari hadi Agosti 2024, wakimbizi 1,655 wamerejea Burundi kwa hiari, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na lengo la kuwarejesha wakimbizi 28,000 katika kipindi cha miezi saba.

“Hadi Agosti 6, 2024 (leo), kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ina jumla ya wakimbizi 134,920.  Wakimbizi 87,190 wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na 47,588 wanatoka Burundi,” amesema Menjenje.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, Daniel Sillo amesema Serikali inatambua kuwa Burundi ina amani kwa sasa, hivyo hakuna sababu ya wakimbizi kushindwa kujiandikisha na kurudi kwao kwa hiari.

 “Tunawahamasisha kwa nia njema kujiandikisha na kurejea nchini kwenu kwa hiari ili muungane na familia zenu, kwani Burundi ni salama kabisa,” amesema Sillo.

Mkuu wa UNHCR Wilaya ya Kasulu, Jean Bosco Ngomoni amesisitiza umuhimu wa kuwaeleza wakimbizi ukweli kuhusu hali halisi ya Burundi ili waondoe hofu ya kurejea na akaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wakimbizi wanarejea kwa hiari.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Nibona Celestin amesema Serikali ya Burundi ipo tayari kufanya lolote kuhakikisha raia wake wanarejea nyumbani kujenga nchi yao.

“Ingawa nchi yetu ilipitia changamoto za amani hapo awali, sasa imerejea na tunahimiza wakimbizi warudi kujenga taifa lao,” amesema Celestin.

Baadhi ya wakimbizi waliorudi Burundi wamesema walichukua uamuzi huo baada ya kuona amani imerejea nchini kwao.

Ramadhani Nzokurishaka, aliyekuwa mkimbizi katika kambi ya Nyarugusu, amesema alikimbia Burundi mwaka 2015 na amerudi Juni 2024, akiwahimiza Warundi wenzake kurudi nyumbani kujenga nchi yao.

Itakumbukwa katika mkutano wa 24 wa pande tatu ulioshirikisha serikali ya Tanzania, Burundi na UNHCR, uliofanyika Novemba 2023, jijini Dar es Salaam, ilikubalika kwamba wakimbizi 2,000 wanapaswa kurejeshwa kila wiki, lakini lengo hilo halijawahi kufikiwa.

Related Posts