Walimu wanaofundisha vijijini walia na mtandao, waiomba NMB kufanya jambo

Lindi. Walimu wanaofundisha shule za vijijini wameiomba Benki ya NMB kusaidia mcahakato wa kuboresha huduma ya mtandao, ili waweze kufanya miamala ya kibenki kwa urahisi.

Akizungumza leo Jumanne, Agosti 6, 2024, katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Benki ya NMB, Mwalimu Nathiri Mbelwa kutoka Shule ya Sekondari Chikonji, Manispaa ya Lindi, amesema benki hiyo inapaswa kuboresha huduma ya mtandao ili kuwasaidia walimu wanaofundisha vijijini kufanya miamala kwa urahisi badala ya kusafiri hadi mjini.

“Sisi walimu tunaofundisha vijijini tunapata shida kwenye suala la mtandao. Benki ya NMB itusaidie kutuwekea mtandao ili tuweze kufanya miamala kwa urahisi zaidi kuliko kuja hadi mjini,” amesema Mbelwa.

Naye Mwalimu Hoja Sefu kutoka Halmashauri ya Mtama, amesema programu ya “Mwalimu Spesho” inayotolewa na benki hiyo inasaidia walimu kuweka akiba na kutekeleza majukumu ya dharura endapo watapata changamoto za kifedha.

“Tunawashukuru Benki ya NMB kwa kutupatia warsha hii ya ‘Mwalimu Spesho’ ambayo itatusaidia sisi walimu kuweka akiba na kutatua changamoto zetu,” amesema Sefu.

Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo amesema programu ya “Mwalimu Spesho” ilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kumsaidia mwalimu kutunza fedha na kutoa masuluhisho mbalimbali, ikiwemo kuondoa changamoto na kuongeza fursa kwa walimu.

“Programu hii ya ‘Mwalimu Spesho’ ilianza tangu mwaka 2022, ambapo benki iliamua kuja na mpango huu ili kumsaidia mwalimu kuondoa changamoto zake na kuweka akiba ya fedha,” amesema Ng’ingo.

Ng’ingo ameongeza kuwa, ndani ya programu hiyo wamewafikia walimu zaidi ya 10,000 kwa mwaka, na wakati wa warsha hizo walimu zaidi ya 200 hufundishwa na kupewa ujuzi wa kuwaelimisha wenzao ambao hawajapata nafasi ya kuhudhuria. Amesema pia wanapanga kupanua programu hiyo ili kuhusisha sekta nyingine kama afya katika miaka ijayo.

“Elimu wanayoipata itawasaidia kuongeza kipato na kwa kufanya hivyo watakuwa na mazingira bora ya utendaji kazi,” ameongeza.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele amewataka walimu kuendelea kutumia benki hiyo kujiwekea akiba ili kutatua changamoto zao.

Benki ya NMB ilitoa warsha ya utunzaji fedha na kuweka akiba kwa walimu wa shule za sekondari, shule za msingi pamoja na maofisa elimu msingi na sekondari katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Related Posts