Waliofaulu usaili wa ajira serikalini waitwa kazini

Dar es Salaam. Watanzania walioomba kazi katika nafasi mbalimbali ambao walifanya usaili kati ya Januari 14, 2023 na Juni 21, 2024 na kufaulu sasa wameitwa kuripoti kazini.

Jana Jumatatu, Agosti 5, 2024, taarifa ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imesema watu hao wanatakiwa kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi ndani ya siku saba kuanzia jana.

“Waombaji waliofaulu usaili wanatakiwa kuchukua barua katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwenye majengo ya Dk Asha Rose Migiro, masjala ya wazi.

“Wanapaswa kuchukua ndani ya siku saba kutoka tarehe ya tangazo hili na baada ya hapo barua ambazo hazitachukuliwa na wahusika zitatumwa kupitia anuani zao za Posta,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika orodha ya majina hayo, pia inajumuisha baadhi ya wasailiwa waliokuwa kwenye kanzidata (Database) kwa kada mbalimbali ambao wamepangiwa vituo vya kazi baada ya nafasi kupatikana.

Aidha, taarifa imeongeza waombaji kazi waliofaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi wanatakiwa kuripoti kwa mwajiri katika muda ambao umeainishwa kwenye barua za kupangiwa kituo cha kazi wakiwa na vyeti halisi za masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira.

“Kwa wale ambao majina yao hayapo katika tangazo hili watambue kuwa hawakupata nafasi/hawakufaulu usaili, hivyo wasisite kuomba kwa mara nyingine nafasi za kazi zitakapotangazwa.”

Aidha imesisitizwa kwa wale wanaokwenda kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi wanapaswa kuwa na kitambulisho ambacho kinakubalika kwa ajili ya utambuzi. Miongoni mwa vitambulisho hivyo ni pamoja na kitambulisho cha uraia, hati ya kusafiria, kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, mpiga kura au leseni ya udereva.

Related Posts