Dar es Salaam. Wamiliki wa mabasi wamelazimika kuegesha baadhi ya mabasi wakitafuta njia mpya baada ya treni ya kisasa ya umeme (SGR) kuanza safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, ikielezwa imevuruga biashara yao.
Kutokana na ugumu wa biashara, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) inapanga kukutana na wanachama wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) ili kuja na njia mpya.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taboa, Mustapha Mwalango amesema tangu SGR ilipoanza safari Julai 25, 2024 mabasi mengi yameathirika baadhi ya wamiliki wamelazimika kuyaegesha.
“Mwanzoni tulipofikiria kuhusu huduma za treni inayotumia umeme tulidhani haitaathiri biashara yetu. Ukweli ni kwamba Watanzania wameipokea na kuielewa SGR kwa kiasi kikubwa,” amesema na kuongeza:
“Kuanzishwa kwa SGR kumechangia kupungua kwa idadi ya abiria na waendeshaji wengi wa mabasi tayari wamepunguza idadi ya mabasi kutokana na idadi ndogo ya abiria. Kwa kweli, baadhi ya mabasi hayana abiria kabisa.”
Amesema safari moja ya treni hubeba kati ya abiria 700 hadi 900 hivyo yangehitajika mabasi kadhaa kusafirisha idadi hiyo ya abiria.
Kwa mujibu wa Mwalango ni robo tu ya idadi ya kawaida ya mabasi yanayosafiri sasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kuwa mabasi hutumia muda mwingi barabarani.
SGR inatumia takribani saa tatu na dakika ishirini kusafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma, wakati umbali huohuo unachukua hadi saa 10 kwa basi.
“Hivyo basi, hatutarajii kushindana na treni inayotumia umeme. Tunachoweza kufanya ni kushirikiana na TRC (Shirika la Reli Tanzania) kuhakikisha operesheni za mabasi zinaendelea kuwepo,” amesema.
Mkurugenzi wa mabasi ya BM Coach, Basiri Makundi akizungumza na gazeti dada la The Citizen amesema tangu kuanza kwa huduma za SGR biashara imeporomoka.
“Kabla ya huduma za SGR kuanza, tulikuwa tunapeleka kati ya mabasi 20 na 22 kwenye njia ya Dar es Salaam-Morogoro kila siku, wakati mengine 10 yalikuwa yanapelekwa kwenye njia ya Dar es Salaam-Dodoma. Sasa tunaendesha mabasi sita tu kwenye njia ya Dar es Salaam-Morogoro na manne tu kwenye njia ya Dar es Salaam-Dodoma,” amesema.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo wanatarajia kuanzisha njia mpya.
Mwakilishi wa Kampuni ya mabasi ya Shabiby, Edward Magawa akizungumza Agosti 5 mwaka huu kwenye kipindi cha runinga cha asubuhi kwenye UTV amesema: “Inapaswa kuona jinsi waendeshaji wa mabasi, ambao pia ni walipakodi, wanaweza kuendelea na biashara.”
Amesema kupungua kwa idadi ya abiria kwenye vituo vya mabasi siyo tu kumewaathiri wao bali pia kumeathiri watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wadogo, wauza chakula na biashara nyingine.
Amesema Shabiby wanachunguza njia ya kupanua biashara kwa kutafuta maeneo mengine badala ya kutegemea njia ya Dar es Salaam-Dodoma.
Magawa ameiomba Serikali kuanzisha vituo vya mabasi karibu na vituo vya SGR ili iwe rahisi kwa abiria kuunganisha au kupata mabasi na kuendelea na safari.
Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano amekiri kuwa biashara ya mabasi imeporomoka.
Amesema wiki mbili kabla ya kuanza kwa huduma za SGR walifanya uchunguzi kwa njia ya Dar es Salaam-Morogoro.
Amesema uchunguzi ulilenga idadi ya mabasi kama inavyofuatiliwa kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Magari (VTS).
“Tulitambua basi ambalo lilikuwa linaanzia Dar es Salaam kwenda Morogoro na kisha kurudi kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam na tena kurudi Morogoro kutoka Dar es Salaam (safari tatu) limepunguza safari hizo kuwa mbili tu (Dar es Salaam-Morogoro na kurudi Dar es Salaam)” amesema.
Amesema idadi ya abiria waliokuwemo kwenye mabasi nayo imepungua kwa asilimia 20.
“Kuhusu njia ya Dar es Salaam-Dodoma, timu ya wataalamu inafanya uchunguzi ili kuona athari za SGR kwenye mabasi na tutakuja na matokeo hivi karibuni,” amesema.
Amesema wiki ijayo wanatarajia kufanya mkutano wa wadau na wasafirishaji na TRC ili kuhakikisha kuna eneo karibu na vituo vya SGR ambalo mabasi yanaweza kuchukua abiria wanapowasili kwa treni.
Hatua hiyo amesema itapunguza mzigo ambao abiria wanakumbana nao wanapounganisha safari baada ya kufika Dodoma na kwa wale wanaosafiri kwenda Singida, Mwanza, Babati na maeneo mengine.
Hata hivyo amesema Latra haifikirii kubadilisha ukomo wa kasi ya mabasi.