Wanachama Chadema wafunguka Wenje kutaka nafasi ya Lissu

Mikoani. Baadhi ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wametoa maoni mseto kufuatia tamko la Ezekia Wenje aliyetangaza nia ya kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho bara.

Wenje ambaye ni mwenyekiti wa Kanda ya Victoria Chadema, ametangaza kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa na Tundu Lissu jana Jumatatu Agosti 5, 2024 jijini Mwanza.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti, 6, 2024,  baadhi ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kutoka Kanda ya Victoria (Mwanza, Kagera na Geita), Kanda ya Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu) na Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma) wamemuunga mkono huku wengine wamkimpinga kugombea nafasi hiyo.

Mwanachama wa Chadema Mwanza, Victor Kikachichi amempongeza Wenje kwa kujitokeza kuwania nafasi hiyo akidai kufanya hivyo ni kudhihirisha chama hicho kinafuata misingi ya kidemokrasia.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Paulo Paulin amesema nafasi hiyo inastahili mtu shupavu na mkongwe, hivyo kutangaza kwake imeonesha ndani ya chama hicho kuna mkanganyiko unaoendelea baina yao.


Wenje atangaza kugombea nafasi ya Lissu amtaja Lema

“Wenje namfahamu tangu akiwa mwalimu Butimba baadaye akawa mbunge wa  Nyamagana, ndani ya chama bado ni mchanga na hii imeonekana kwenye chama kuna mgawanyiko ila kwa makamu mwenyekiti nafasi hiyo haimfai na hastahili,”amesema.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Peter Francis amesema nafasi ya makamu mwenyekiti anatakiwa kuwa mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi na anayeweza kuhimili  changamoto za chama.

“Katika mazingira ya kawaida inawezekana lakini kiuhalisia Wenje hana uwezo wa kumudu hiyo nafasi kwa sababu hata age (umri) inachangia, nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi kwa hiyo mimi nashauri agombee ubunge lakini hiyo nafasi hatoivaa ipasavyo,” amesema.

Mwenyekiti Chadema Tabora, James Kabepele amesema alichokifanya Wenje kimetafsiri na kuwapa majibu waliodhani hakuna demokrasia ndani ya chama hicho.

“Kinachofanywa na Wenje inatupa heshima kwa kiasi kikubwa na sio Wenje pekee ambaye anaweza kugombea tunakaribisha wengine kugombea nafasi za uongozi kwenye chama chetu,” amesema.

Mkazi wa Tabora, Hamida Ally amesema ameonesha ukomavu wa kisiasa pamoja na ujasiri akidai nafasi anayoitaka kwa sasa inashikiliwa na mtu mwenye umaarufu ndani na nje ya chama hicho.

Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Silvester Lugembe amesema Wenje katumia vizuri  katiba ya Chadema inayotoa nafasi kwa mwanachama yeyote kuchagua.

 “Kama kulivyo na ushindani kwenye chaguzi za chini basi hata za juu demokrasia inapaswa iwepo kwa sasa chama kina zaidi ya miaka 30 kimeonyesha ukomavu wa kiasiasa ni haki ya kidemokrasia kwa mwanachama yeyote atakayetaka kugombea hata nafasi ya mwenyekiti wanaoona wana sifa wanaweza kujitokeza kugombea,”amesema Katibu wa Chadema Mkoa wa Geita, Deo Shinyanga.

Maoni kama hayo yametolewa pia na Pasquina Ferdinand kutoka Geita akisema endapo jina lake litapitishwa na halmashauri kuu ya chama hicho, watamuunga mkono kwa kuwa chama kimejengwa kwenye misingi ya demokrasia na mtu kutangaza nia ni haki yake.

 Uamuzi wa Wenje pia, umeungwa mkono na wanachama mkoani Mara wakidai anafaa kwa nafasi hiyo na ana misimamo thabiti isiyoyumba.

“Ni mfia chama ana weza kufanya vizuri, misimamo yake ni kama mtangulizi wake kwa hiyo apewe  nafasi,  naamini kwa kushirikiana na mwenyekiti watakifikisha chama sehemu sahihi,” amesema Fazel Janja, mkazi wa Geita

Naye, Eliya Magafu amesema umefika wakati wanachama wengine kupewa nafasi kuongoza akidai changamoto ya kidemokarasia imetolewa na Wenje na anachotakiwa kufanyiwa ni kupewa nafasi na sio kubanwa.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Samwel John amesema uwezo wa mtu unapimwa kutokana na uzoefu alionao.

“Uzoefu wa Wenje Chadema unaonesha amekomaa katika siasa na kimsingi ametimiza takwa la kikatiba na endapo Tundu Lissu atagombea nafasi hiyo tena wanakwenda kuleta hamasa kubwa kwa wapigakura na mwisho wa siku wataamua ni nani anayewafaa pamoja na kwamba lissu anakubalika zaidi yake,” amesema Samwel.

Imeandikwa na Beldina Nyakeke (Mara), Timothy Lugoye (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Johnson James (Tabora) na Samwel Mwanga (Simiyu).

Related Posts