Taarifa iliyotolewa Jumanne na maafisa wa wizara ya afya ya Palestina imeeleza kuwa waliouawa ni pamoja na vijana wanne, wawili wakiwa na umri wa miaka 19 na mwingine mwenye umri wa miaka 14, ambao waliauwa katika shambulizi la usiku wa kuamkia Jumanne kwenye kijiji cha Aqaaba kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
Jeshi la Israel halijazungumzia tukio hilo
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kijana mwingine mwenye umri wa miaka 18, aliuawa katika shambulizi jengine tofauti huko Jenin. Watu wengine saba wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. Hakuna taarifa yoyote ambayo imetolewa na jeshi la Israel kuelezea mauaji hayo.
Ama kwa upande mwingine, duru za kiusalama na afya zimeeleza kuwa shambulizi la Israel lililofanyika leo katika mji wa Mayfadoun, kusini mwa Lebanon limewaua watu wanne. Duru hizo zimeeleza kuwa watu wote wanne waliouawa ni wanaume. Huku makabiliano mengi ya risasi kati ya kundi la wanamgambo la Lebanon, Hezbollah na jeshi la Israel yakiwa yanafanyika tu katika eneo la mpaka, mji wa Mayfadoun uko umbali wa kilomita 30 kaskazini mwa mpaka wa Lebanon na Israel.
Iran yatetea haki yake kuiadhibu Israel
Wakati huo huo, Iran imetetea haki yake ya kuiadhibu Israel, kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh, mjini Tehran, wiki iliyopita.
Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kanaani, amesema Iran haitaki kuendeleza mzozo wa kikanda katika Mashariki ya Kati, lakini ina haki kisheria kuiadhibu Israel. Kanaani pia ameitolea wito Marekani kuacha kuiunga mkono Israel na badala yake iunge mkono adhabu kwa nchi hiyo ambayo ni mchokozi.
Soma zaidi: Iran: Tunayo haki ya kuiadhibu Israel kufuatia mauaji ya Haniyeh
”Kwa bahati mbaya, katika kipindi cha miezi 10, serikali ya Marekani imekuwa ikifanya kila iwezalo kuisaidia Israel kufanya uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina ambao wanakandamizwa,” alisisitiza Kanaani.
Afisa huyo amesema ni wajibu wa serikali ya Marekani kuishinikiza vikali Israel ili ikomeshe mzozo huu na kuzuia mauaji yanayofanywa na Israel, na kwamba zaidi ya hayo, Marekani inapaswa pia kuacha kuipatia Israel silaha za maangamizi,” alisisitiza Kanaani.
Huku hayo yakijiri, Rais wa Marekani Joe Biden, Jumatatu alizungumza kwa njia ya simu ya Mfalme Abdullah II wa Jordan, ambapo wamejadiliana kuhusu juhudi za kuzuia kuongezeka kwa mzozo katika Mashariki ya Kati. Biden na Mfalme Abdullah walijadiliana kuhusu kumaliza vita kati ya Israel na Hamas na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza.
Imeripotiwa kuwa katika siku za hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman al-Safadi, alisafiri kwenda Tehran kwa mazungumzo na waziri mwenzake Ali Bagheri, ambapo alijaribu kuwashauri viongozi wa Iran kutolipiza kisasi kwa Israel.
Aidha, serikali ya Lebanon imesema inajaribu kulizuia kundi la Hezbollah kujibu mashambulizi kwa Israel, hatua ambayo inaweza kuanzisha vita vikubwa.
(AP, AFP, DPA, Reuters)