Wapinzani nchini Venezuela wachunguzwa – DW – 06.08.2024

Mwendesha mashtaka mkuu waVenezuela ametangaza juu ya kuanzishwa uchunguzi wa makosa ya jinai dhidi ya mgombea urais Edmundo Gonzalez na kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado juu ya wito wao kwa vikosi vya jeshi kuacha kumuunga mkono Rais Nicolas Maduro na pia kuacha kuwakandamiza waandamanaji.

Soma Pia: Umoja wa Ulaya wasema ushindi wa Maduro hauwezi kutambulika 

Waendesha mashtaka wamesema viongozi hao wa upinzani walimtangaza mshindi mwingine na sio Nicolas Maduro katika uchaguzi wa Rais uliomalizika, hatua ambayo wanasema imechochea uasi na uvunjaji wa sheria.

Venezuela Caracas | Kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado
Kushoto: Mgombea urais wa Venezuela Edmundo Gonzalez Urrutia. Kulia: Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Maria Corina Machado Picha: Federico Parra/AFP/Getty Images

Wakati umma nchini Venezuela unasisitiza kutolewa mjumuisho wa kina wa taarifa kuhusu ushindi wa Maduro, Baraza la Taifa la Uchaguzi limesema limewasilisha orodha zote kwa Mahakama ya Juu nchini Venezuela kwa ajili ya kuthibitishwa, kama jinsi alivyoomba Rais Nicolas Maduro ambaye ametaka majumuisho hayo yasifanyike hadharani.

Wakati huo huoRais wa VenezuelaNicolas Maduro amesema ataachana kabisa na mtandao wa kijamii wa WhatsApp, akiwahimiza watu wengine kufanya vivyo hivyo, kwa sababu amesema programu hiyo inatumiwa kuzitishia familia za wanajeshi na maafisa wa polisi nchini mwake.

Serikali ya Maduro imekuwa chini ya shinikizo la kitaifa na kimataifa tangu mamlaka ya uchaguzi ya Venezuela, ilipomtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi wa Julai 28 huku ikikataa kuzionesha hesabu za kura.

Uchaguzi Venezuela 2024 | Nicolas Maduro na Edmundo Gonzalez Urrutia
Kushoto: Rais wa Venezuela Nicolas Maduro. Kulia: Mpinzani aliyegombea urais Edmundo Gonzalez Urrutia Picha: Yuri Cortez/AFP/Rances Mattey/Anadolu/picture alliance

Upinzaniumesisitiza kuwa Edmundo Gonzalez Urrutia, ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa rais ambao umeliingiza taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta katika mgogoro wa kisiasa.

Soma Pia:  Mataifa ya ulaya yaitaka Venezuela kuweka wazi nyaraka za uchaguzi

Upinzani umesema hesabu zinaonesha mgombea Edmundo Gonzalez inawezekana alipata asilimia 67 ya kura, akiwa ameshinda kwa karibu kura milioni 4, na hivyo kuwashinda kwa zaidi ya mara mbili waliomuunga mkono Maduro, kulingana na matukio huru ya awali yaliyotolewa.

Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Argentina, zimemtambua Edmundo Gonzalez kama mshindi, huku nyingine, kama vile Umoja wa Ulaya, zikitoa wito wa kuchapishwa matokeo kamili kulingana na kura zilivyopigwa.

Venezuela Maandamano kupinga matokeo ya kura
Mbele Kushoto: Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado na wenzakePicha: Cristian Hernandez/AP/picture alliance

Uchaguzi wa Rais wa Venezuela ulikuwa na ushindani mkali na matokeo yake yalizusha maandamano wiki iliyopita ambapo takriban raia 11 walipoteza maisha kwenye maandamano hayo, kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Vyanzo: AP/DPA/AFP

 

 

Related Posts