Washangilia mtaani kukimbia kwa waziri mkuu

 

MAELFU ya watu wamejimwaga barabarani kusheherekea kujiuzulu kwa waziri mkuu wa Bangladesh, Bi. Sheikh Hasina, kufuatia wiki kadhaa za maandamano mabaya dhidi ya serikali yake. Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).

Maandamano hayo yaliyoanzishwa na vuguvugu la wanafunzi kupinga mfumo wa upendeleo wa nafasi za kazi serikalini, yamekomesha miongo kadhaa ya utawala wa familia hiyo, katika siasa za nchi hiyo.

Vyombo vya habari nchini Bangladesh vinaripoti kuwa Sheikh Hasina, amekimbilia nchini India, na baadaye anaelekea London, baada ya waandamanaji kukaidi amri ya kutotoka nje na kuvamia makaazi yake mjini Dhaka.

Hasina (76), ameitawala Banglashi tangu mwaka 2009 na alishinda muhula wa nne mfululizo Januari mwaka huu, kwenye uchaguzi uliosusiwa na upinzani.

Serikali yake ilituhumiwa na mashirika ya haki za binadamu, kutumia vibaya taasisi za serikali kujiimarisha madarakani na kuzima upinzani, ikiwemo mauaji dhidi ya wanaharakati wa upinzani.

Mapema jana Jumatatu (tarehe 5 Agosti), maelfu ya waandamaji walilivamia kasri la waziri mkuu huyo baada ya duru kufahamisha kuwa ameikimbia nchi kufuatia maandamano makubwa ya kumshikiza ajiuzulu.

Kituo cha televisheni cha Chanel 24 kilionesha picha za makundi ya waandamanaji wakikimbilia kuingia ndani ya makaazi ya waziri mkuu katika mji mkuu Dhaka.

Baadhi ya waandamanaji walionekana wakijaribu kubomoa sanamu ya kiongozi wa uhuru Sheikh Mujibur Rahman, baba yake Bi Hasina.

Kabla ya waandamanaji kuvamia kasri la waziri mkuu, mtoto wa kiume wa Hasina alikuwa amevitaka vikosi vya usalama kuzuia utwaaji wowote wa madaraka kutoka utawala wa miaka 15 wa mama yake.

Saa chache baada ya Bi Hasina kujiuzulu, Rais Mohammed Shahabuddin aliamuru kuachiliwa kwa waziri mkuu wa zamani Khaleda Zia aliyefungwa jela na wanafunzi wote waliokuwa wamezuiliwa wakati wa maandamano hayo.

Rais Shahabuddin alisema alikuwa ameongoza mkutano wa wakuu wa jeshi na wawakilishi wa kisiasa. Akaahidi kuundwa kwa serikali ya mpito, uchaguzi mpya kuitishwa na amri ya kutotoka nje ya kitaifa kuondolewa.

Mjini Dhaka siku ya Jumatatu, polisi na majengo mengine ya serikali yalishambuliwa na kuchomwa moto.

Vikosi vya jeshi na polisi vilisambazwa katika jiji lote. Huduma ya simu za mkononi iliripotiwa kukatika kwa saa kadhaa kabla ya kurejeshwa.

Katika ghasia hizo, makumi waliripotiwa kuuawa jana Jumatatu, ingawa idadi kamili bado haijafahamika.

Shirika la habari la AFP lilitaja waliofariki kuwa watu 66, ingawa shirika la habari la Dhaka Tribune, lilisema kuwa watu 135 wameuawa.

Kabla ya waandamanaji kujibwaga mitaani kusheherekea ushindi, katika baadhi ya maeneo walionekana kwenye video wakiwa wamebeba silaha, huku jeshi likishika doria katika mitaa ya mji mkuu.

Watu wasiopungua 94 waliuawa hadi Jumapili iliyopita, wakiwemo maafisa 14 wa polisi. Waandamanaji na wafuasi wa serikali walipambana kote nchini humo kwa kutumia visu na fimbo, na vikosi vya usalama vikatumia risasi za moto.

Vurugu hizo za jana zilifikisha idadi jumla ya watu waliouawa katika maandamano yalioanza mwanzoni mwa Julai kufikia siyo chini ya 300, kwa mujibu wa hesabu za AFP zilizokusanywa kutoka polisi, maafisa wa serikali na madaktari hospitalini.

About The Author

Related Posts