Watuhumiwa ‘waliotumwa na afande’ wakamatwa

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema tayari vyombo vya dola vimeshawatia nguvuni watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti wa msichana anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.

Agosti 4, 2024 zilisambaa video katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimtuhumu kwa kile kilichosikika katika video hiyo kuwa ametembea na mume wa mtu.

Kadhalika, katika video hiyo inayodaiwa kuchukuliwa na vijana hao, binti huyo alisikika akieleza anakotokea na kumwomba msamaha mtu aliyetambulishwa kwa jina la afande.

Masauni amethibitisha kutiwa nguvuni kwa vijana hao leo, Jumanne Agosti 6, 2024 alipotafutwa na Mwananchi Digital kwa njia ya WhatsApp.

Katika ujumbe mfupi aliotumiwa kuulizwa iwapo watuhumiwa hao wameshakamatwa, Masauni alijibu kwa kuandika “tayari” kupitia ujumbe huohuo wa njia ya WhatsApp.

Hata hivyo, Waziri Masauni hajafafanua zaidi kwani amesema bado yupo kwenye mkutano kwa sasa.

Miongoni mwa wadau walioshinikiza Serikali kuchukua hatua ni Meya wa zamani wa Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob kupitia mtandao wake wa X (zamani Twitter), aliyeelezea tukio hilo na kuwaomba viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuchukua hatua.

Jioni ya jana Jumatatu Agosti 5, 2024, Mwananchi ilimtafuta Waziri Masauni kujua hasa nini kinaendelea juu ya watuhumiwa hao, akasema vyombo vinavyohusika vinaendelea kulishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.

“Tupo tunalishughulikia. Mchakato unaendelea wa kuwakamata na kuhakikisha tunawapeleka kwenye vyombo vya sheria,” amesema Masauni.

Endelea kufuatilia tovuti ya Mwananchi

Related Posts