Alama hiyo ilionekana kwenye video zilizotolewa na vikosi vya Wapalestina vya Al-Qassam ambalo ni tawi la jeshi la wanamgambo wa Hamas, kutanabahisha shabaha za kijeshi za Israeli, kama vile vifaru, muda mfupi baada ya wanajeshi wa Israeli kuingia kwenye Ukanda wa Gaza.
Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa zimeiorodhesha Hamas kuwa ni kundi la kigaidi.
Baada ya mashambulio ya Hamas ya mwezi Oktoba mwaka 2023,ndani ya Israel, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani alipiga marufuku shughuli zote za kundi hilo nchini Ujerumani.
Mjini Berlin, alama hiyo ya pembe tatu imechorwa kwenye maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kwenye klabu ya techno na kwenye baa moja ambako matukio ya kupinga chuki dhidi ya Wayahudi yalifanyika pia kwa madhumuni ya kuonyesha mshikamano na Israel baada ya mashambulio ya Oktoba 7.
Soma pia:Mahakama Ujerumani yapiga marufuku chama cha itikadi kali cha Heimat kupokea ruzuku ya serikali
Polisi wa jiji la Berlin hawawezi kuhesabu ni mara ngapi alama hiyo imetumika kwa namna hiyo.
Pembe tatu ya rangi nyekundu ambayo haikugeuzwa chini juu pia inaonekana katika bendera ya Palestina, inatoyokana na muundo wa kitaifa kutoka mwaka 1916.
Lakini waandamanaji wanapoivaa bendera hiyo kwenye mabega yao au ikiwa wameitundika wima madirishani, huonekana imegeuzwa.
Alama hiyo imeonekana katika muktadha tofauti kwenye maandamano ya Wapalestina kote ulimwenguni, pamoja na katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin. Ishara hiyo inaonekana kwenye mitandao ya kijamii na kwenye maaandamano ya kupinga vita.
Mapema mwezi Julai, seneti ya jimbo la Berlin ilipitisha hoja ya dharura ili kuupanua wigo wa kuipiga marufuku Hamas na pia kuijumuisha alama ya pembe tatu nyekundu.
Kutumia alama za mashirika yanayopinga katiba au alama za mashirika ya kigaidi ni kosa linaloweza kumfanya atakayepatikana na hatia afungwe kifungo cha hadi miaka mitatu jela hapa nchini Ujerumani.
Hoja zinazotumika kutaka kuipiga marufuku alama
Hoja iliyowasilishwa na baraza la seneti katika jiji la Berlin inasema wanaoyaunga mkono mashirika ya kigaidi ya Palestina waliitumia alama ya pembe tatu nyekundu kuashiria maeneo yanayolengwa kushambuliwa.
Hoja ya serikali ya jiji la Berlin inaongezea kusema kuwa alama hiyo ni tishio kwa usalama na utulivu wa umma na kwamba inasababisha hofu hasa katika jamii ya Wayahudi.
Lengo la baraza la seneti la jiji la Berlin ni kuzuia matumizi ya alama hiyo katika muktadha wa Hamas na mgogoro wa Mashariki ya Kati na kwa hivyo matumizi yake ni kosa linaloweza kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za Ujerumani.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani sasa inalizingatia suala hilo katika ngazi ya kitaifa.
Soma pia:Ujerumani yapiga marufuku kundi la Kinazi Mamboleo la Nordangler
Hata hivyo nchini Ujerumani alama ya pembe tatu nyekundu inajulikana kuwa ishara ya wakati wa utawala wa manazi ambayo baadae ilitumiwa na wahanga wa ufashisti, ingawa imekuwa mara kwa mara ikizingatiwa kuwa alama ya Hamas.
Kutokana na hali hiyo asasi na mashirika ya kupambana na ufashisti ya nchini Ujerumani yamewalaumu wanasiasa kwa kusahau historia. Baadhi ya mashirkka hayo yameshtushwa kutokana na jinsi alama hiyo inavyotumiwa vibaya.
Baada ya kumalizika vita vikuu alama ya pembe tatu nyekundu ilitumiwa na walionusurika maangamizi ya mafashisti kama ishara ya kupambana na ufashisti. Kuhusu mjadala wa kuipiga marufuku alama hiyo wapo wanaotilia mashaka.
Mkurugenzi wa taasisi ya Max Planck, Ralf Michaels, amesema alama kama hiyo inaweza kuwa na maana mgawanyiko amesema haina maana kwamba inapotumiwa na upande fulani inamaanisha kuunga mkono ugaidi na inapotumiwa na upande mwingine iwe na maana tofauti!