Dar es Salaam. Bei ya petroli na dizeli ya rejareja kwa Agosti 2024 imepanda katika mikoa inayochukua mafuta hayo kwenye bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na Julai.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei za mafuta kuanzia leo Jumatano Agosti 7, 2024 kwa yanayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam, petroli imepanda kwa Sh21 kwa lita moja na kuwa Sh3,231
Pia, kwa petroli inayochukuliwa katika Bandari ya Tanga, kwa lita moja imepanda kutoka Sh3,210 Julai hadi Sh3,229 Agosti na kwa Bandari ya Mtwara imepanda hadi Sh3,304 kutoka Sh3,212 Julai.
Kwa upande wa bei ya dizeli, taarifa ya Ewura inasema bidhaa hiyo inayopokewa Bandari ya Dar es Salaam bei yake imeongezeka kutoka Sh3,115 Julai hadi Sh3,131 Agosti.
Na dizeli inakayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka kutoka Sh3,124 Julai hadi Sh3,138 na Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,124 hadi Sh3,140 Agosti kwa lita.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule, imetaja mwenendo wa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kuongezeka kuwa miongoni mwa sababu ya kupaa kwa bidhaa hizo muhimu katika uchumi.
“Bidhaa za mafuta zinazoagizwa na kupokewa hapa nchini zinazingatia bei za mafuta katika soko la Uarabuni kwa bidhaa zenye viwango vya ubora vinavyokubalika nchini.
“Agosti 2024, bei kikomo za mafuta zimekokotolewa kwa kuzingatia bei za soko la Uarabuni za Julai 2024. Kwa kulinganisha na bei za Juni 2024, bei ya petroli imeongezeka kwa asilimia 6.3 dizeli imeongezeka kwa asilimia 2.2,”inaeleza sehemu ya taarifa hiyo
Pia, imeeleza kuwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 3.58 kwa petroli na asilimia 4.35 kwa dizeli na kupungua kwa asilimia 7.45 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, zimepungua kwa wastani wa asilimia 6.75 kwa petroli na dizeli katika Bandari ya Tanga; na pia zimepungua kwa wastani wa asilimia 7.54 kwa mafuta ya petroli na dizeli katika Bandari ya Mtwara.