ALIYEKUWA Kocha wa Simba msimu uliopita, Mualgeria Abdelhak Benchikha amekifuatilia kikosi kipya cha timu hiyo ya Msimbazi kisha kutoa neno, akiitabiria kufanya maajabu msimu wa 2024-2025.
Kocha huyo mwenye misimamo na maamuzi magumu alijiunga na Simba, Novemba mwaka jana kabla ya kuachia ngazi Aprili 2024 mwaka huu mara baada ya Dabi ya Kariakoo iliyoisha kwa Simba kulala 2-1 mbele ya Yanga kwa kilichoelekezwa alikuwa na matatizo ya familia na Julai akatangazwa kocha wa JS Kabylie.
Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha alisema licha ya kuondoka Simba lakini amekuwa akifuatilia kwa karibu timu hiyo hususani usajili mpya na anaamini itafanya vizuri msimu ujao.
“Nilikuwa Simba na niliishi vizuri katika timu hiyo hivyo siwezi kuacha kuifuatilia. Nina marafiki hapo na tayari imekuwa kama familia yangu katika soka. Nimeona usajili uliofanyika, ni mzuri ni timu inayojengeka upya na naamini itatulia na kufanya vizuri katika msimu ujao,” alisema Benchikha.
Aidha kocha huyo ameweka wazi sababu za kuamua kuwasajili JS Kabyilie viungo wawili waliokuwa Simba, Babacar Sarr na Sadio Kanoute.
“Nilitamani kuendelea kufanya kazi na wachezaji wengi wa Simba, lakini nilipata matatizo yaliyonifanya kuondoka ndani ya klabu hiyo na kurejea nyumbani ili niweze kuyatatu kwa ukaribu. Sarr na Kanoute ni miongoni mwao kwani wanauwezo na nidhamu ya juu. Nafurahi nimeungana nao tena huku na naamini watasaidia katika kutimiza malengo, mpira wa miguu ndivyo ulivyo, kukutana kupo” alisema Benchikha.
Katika hatua nyingine kocha huyo aliizungumzia timu aliyonayo ya JS Kabylie kwa kusema imejipanga kurejea kwenye nafasi za juu na kutwaa mataji mbalimbali.
“Nimefurahishwa na usajili tulioufanya na sasa nadhani ni muda wa kufanya kazi na kuhakikisha tunafanya vizuri na kutwaa mataji,” alisema Benchikha.
Baada ya Benchikha kuondoka Simba, nafasi yake ilikaimiwa na Juma Mgunda kabla ya Wekundu hao kumtangaza Msauzi Fadlu Davids, kuwa kocha mkuu akiambatana na wasaidizi wake jambo lililopelekea Mgunda kuondolewa kikosini hapo na kubaki Seleman Matola.