Dabo aonya mastaa Azam, aitamani fainali ya Ngao

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amewatahadharisha wachezaji wa kikosi hicho wakati wakijiandaa na mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union kesho, utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.

Timu hizo zitakutana katika mchezo huo wa utangulizi utakaopigwa saa 10:00 jioni, kisha baadae kupigwa nusu fainali ya pili ya ‘Kariakoo Dabi’, kati ya Yanga dhidi ya Simba saa 1:00 usiku, mechi itakayofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti Dabo amesema, anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Coastal Union huku akiwataka wachezaji wa timu hiyo kuongeza juhudi zaidi ili wapate matokeo chanya na kuacha tabia za kimazoea kutokana na rekodi zao kwa wapinzani wao.

“Tumecheza na Coastal Union mara tatu msimu uliopita na licha ya kupata matokeo mazuri lakini imekuwa timu inayotupa wakati mgumu sana kimbinu, wachezaji wanahitaji kuonyesha jinsi gani wanauhitaji mchezo ili tupate kilichokuwa bora,” amesema na kuongeza;

“Unapocheza hatua kama hizi maana yake kila mmoja anahitaji ubingwa na hata sisi pia kama Azam FC ndio kiu na shauku yetu kwa sababu tuna wachezaji bora wanaoweza kuipigania timu, tunaiendea mechi moja baada ya nyingine hivyo mawazo na akili zetu kwa sasa ni mchezo dhidi ya Coastal Union.”

Azam inaingia katika mchezo huo ikitoka kutwaa ubingwa wa michuano ya ‘Choplife Cup 2024’, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na beki, Lusajo Mwaikenda dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda iliyowaalika matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam katika sherehe zao za ‘Rayon Sports Day’, zilizofanyika Agosti 3, mwaka huu.

Timu hiyo imedhamiria kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwani tangu mwaka 2001, Azam FC imechukua taji hilo mara moja tu ambao ilikuwa mwaka 2016, ilipoifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1, baada ya sare ya mabao 2-2.

Hili ni pambano la 24 kwa timu hizo katika mashindano yote tangu 2011, na kwa mechi 23 zilizopita Azam imeshinda 13 ikiwamo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita iliyochezwa CCM Kirumba, Mwanza ilipoitambia kwa mabao 3-0, huku Wagosi wakishinda nne tu na nyingine sita zikiisha kwa sare.

Related Posts