Dar es Salaam. Ili kukabiliana na changamoto ya madeni ya bili za maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imejipanga kuwafungia dira za maji za malipo ya kabla wadaiwa, ikieleza mpaka sasa inawadai zaidi ya Sh40 bilioni.
Kwa mujibu wa Dawasa, wadaiwa hao wapo katika makundi matatu ambayo ni taasisi zinazodaiwa Sh22 bilioni, walioondolewa kwenye huduma wakidaiwa Sh15 bilioni na wateja wanaoendelea kupata huduma wakidaiwa Sh10 bilioni.
Hatua hiyo inatokana na matumizi ya dira za maji zaidi ya 200 kwa majaribio ya miezi sita katika maeneo ya Mikocheni, Oysterbay Polisi na Tegeta ambazo zimeonyesha mafanikio, hivyo kupunguza madeni.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari leo Agosti 7, 2024 jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema dira hizo za maji zitasaidia katika ufuatiliaji na ulipaji wa madeni.
“Tukishafunga mita za malipo ya kabla zitasaidia katika uboreshaji wa huduma, kwani hakutakuwa na muda wa kwenda kusoma mita wala ufuatiliaji wa madeni,” amesema Bwire.
Amesema ili kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi, watashirikiana na sekta binafsi ambayo ameitaka kuiona fursa hiyo na kuwezesha kazi kufanyika kwa kasi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amewaomba Dawasa kuwaangalia wajasiriamali vijana wanaotengeneza mita za maji kwa kuwapa zabuni.
“Tunajua mnaagiza mita kutoka nje ambazo nyingine hazina ubora, ili kupunguza gharama kuna vijana wanatengeneza mita hapa nchini wapeni tenda ya kufanya kazi hiyo. Tunajua mliwaambia watengeneze 50 kwanza, hivyo muwafikirie,” amesema Balile.
Akizungumzia upotevu wa maji, Bwire amesema wamejipanga kwa miaka mitatu kuhakikisha unakuwa himilivu wa chini ya asilimia 30 kwa kuhakikisha wanaimarisha utambuzi wa maeneo yenye kuvuja na pia kuhakikisha hatua zinachukuliwa haraka kurekebisha maeneo yenye changamoto.
Katika kutekeleza hilo, amesema wataongeza uwajibikaji kwa kupima utendaji wa watumishi wa Dawasa ambao kwa kila maeneo ya utawala, watafunga mita kubwa ili kufanya ufuatiliaji wa kiasi cha maji yanayohitajika na yaliyotumika.
Hatua hiyo amesema pia itasaidia kukabiliana na upotevu wa maji.
Bwire akizungumzia utendaji kazi kwa miaka mitatu (2021/22- 2023/24), amesema miradi kadhaa yenye thamani ya Sh495.6 bilioni baadhi imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa, ili kukabiliana na mahitaji ifikapo mwaka 2050.
Dawasa inahudumia mikoa ya Dar es Saalam na Pwani, pamoja na sehemu ya Morogoro (Ngerengere, Gwata) na Tanga (Kwasunga).
Amesema Mkoa wa Pwani unakua kwa kasi, hivyo matumizi ya maji nayo yanaongezeka, ikiwamo viwandani na kwamba wanajipanga kutosheleza mahitaji.
Miongoni mwa miradi hiyo amesema ni wa bwawa la Kidunda lililopo Morogoro Vijijini ambalo utekelezaji wake umefikia asilimia 21 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026, huku ukigharimu Sh329 bilioni.
Amesema bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo bilioni 190 na pia kutajengwa mtambo wa kuzalisha umeme megawati 20 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mradi mwingine wa muda mrefu ni wa kuzalisha maji kutoka Mto Rufiji.