DC Batenga: Tumuenzi Sauli kwa kuendeleza miradi yake

Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga amesema njia bora ya kumuenzi aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila ni kuendeleza miradi yake ili kulinda ajira za vijana.

Batenga ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 7, 2024 wakati wa maziko ya Mwalabila yaliyofanyika katika makaburi ya kijijini kwao Godima, wilayani Chunya.

Batenga amesema pamoja na maumivu, masikitiko na huzuni za kumpoteza mdau huyo wa maendeleo, lakini wakumbuke kwamba aliyeondoka ni mtu na si kampuni zake. Amesema Mwalabila maarufu Sauli alikuwa dira kubwa katika kutunza familia yake na kuendeleza maendeleo ya Taifa kwa kufanya uwekezaji na njia bora ya kumuenzi ni kulinda miradi yake.

“Mimi kama mkuu wa wilaya nitafarijika kuona miradi aliyoanzisha Sauli inaendelea kwa ajili ya kulinda ajira za vijana. Aliyeondoka ni mtu, ila mali zake zote ameziacha, tuzilinde,” amesema Batenga.

Pia, amesema familia ya marehemu yenye watoto 16, inahitaji usaidizi wa karibu na uwekezaji aliouweka ulikuwa na lengo la kuihudumia hadi mwisho. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kampuni zake.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Joshua Mlambalala amesema ingawa marehemu alihamishia makazi yake jijini Mbeya, heshima ya kuweka msiba nyumbani kwake imewapa faraja wakazi wa Chunya.

Amesema mchango wa wananchi katika msiba huo umeonyesha mshikamano wa pamoja na ameihimiza jamii kuiga mfano wa maisha ya Sauli.

Mlambalala amesema Sauli aliamua kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupambania uhai wa mama yake ambaye bado anaumwa, lakini Mungu aliamua kumchukua yeye na kumuacha mama huyo ambaye anahitaji uangaliza mkubwa sambamba na matibabu.

Related Posts