Dk Nchimbi awaweka mtegoni mawaziri watano

Kigoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amehitimisha ziara ya siku tatu mkoani Kigoma, alikotoa maelekezo kwa mawaziri watano kushughulikia kero zilizoibuliwa na wananchi.

Dk Nchimbi aliyeanza ziara mkoani humo Agosti 4, 2024 amefanya mikutano kadhaa, akitoa maelekezo kwa mawaziri kushughulikia kero za wananchi wa Kigoma hasa za umeme, usalama wa raia na mali zao, maji na kituo cha afya.

Katika ziara hiyo, Dk Nchimbi ameambatana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM ambao ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Oganaizesheni, Issa Haji Gavu, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, kusikiliza kero za wananchi na kukagua maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Jana Jumanne, Agosti 6, 2024, Dk Nchimbi alihitimisha ziara yake mkoani humo na leo Jumatano, anaingia mkoa jirani wa Kagera atakapofanya ziara ya siku nne hadi Agosti 10, 2024. Atakwenda Geita atakaa hadi Agosti 13 kisha Mwanza atatapotumia siku mbili hadi Agosti 15 na atamaliza ziara mkoani Mara Agosti 18, 2024.

Katika ziara mkoani Kigoma, Dk Nchimbi alipokea kero mbalimbali na kuzitolea maelekezo ya utekelezaji kwa viongozi kadhaa wakiwamo mawaziri ambao ni Hamadi Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani), Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Ujenzi), Jumaa Aweso (Maji), Mohamed Mchengerwa (Tamisemi) na Dk Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Maelezo mengi kwa mawaziri hao ni kutekeleza maagizo ya mtendaji mkuu huyo wa chama tawala kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Lengo ni kutokifanya chama hicho kushindwa kujieleza kwa wananchi kwa nini kimeshindwa kutatua kero zao.

Dk Nchimbi akizungumza na wananchi wa Mwandiga, Jimbo la Kigoma Kaskazini, alikosimama kuwasalimia akiwa njiani kuelekea Wilaya ya Kasulu, alitoa maelekezo kwa Waziri wa Nishati, inayoongozwa na Dk Doto akiitaka wizara hiyo iongeze kasi katika kusambaza umeme kwenye ngazi ya vitongoji baada ya kumaliza vijiji vyote nchini.

Dk Nchimbi alimwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhakikisha kinajengwa kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao eneo la Mwandiga na maeneo mengine ya jirani jimboni humo.

Wananchi walionyesha uhitaji huo kupitia mabango wakati wakimpokea katibu mkuu huyo wa CCM, pia kutokana na maombi ya mbunge wao, Assa Makanika alipokuwa akizungumzia maendele ya jimbo hilo.

“Wakati naingia hapa nimeona mabango, watu wangu wameyachukua kuyafanyia kazi. Mojawapo ya bango lililonifurahisha sana, limesema mnahitaji kituo cha polisi. Imenipatia furaha kwamba ninyi ni watu wema sana. Watu wabaya, majambazi, wezi au wakabaji hawawezi kuomba kituo cha polisi.

“Namwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ahakikishe kituo cha polisi kinajengwa hapa kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Sasa RC (Mkuu wa Mkoa wa Kigoma) kwa kushirikiana na waziri, wananchi wajengewe kituo cha polisi hapa,” amesema Dk Nchimbi.

Pia, ametoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, aliyewakilishwa na Naibu wake, Zainabu Katimba, akimwelekeza afikishe maelekezo kwa waziri kuhusu mahitaji ya kujengwa kituo cha afya kwa ajili ya Tarafa ya Mwandiga.

“Naibu waziri nakupongeza kwa maelezo yako mazuri sana. Hili la kituo cha afya umelisemea vizuri tayari lakini maelekezo hapa ni kwamba, habari za mchakato zimeisha, wananchi hawa wajengewe kituo cha afya kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Naomba utufikishie kwa waziri ambaye pia ni mchapakazi mzuri,” amesema.

Maelekezo mengine aliyaelekeza kwa Wizara ya Maji inayoongozwa na Aweso kutokana na wananchi kumpatia taarifa kuwa, mtandao wa maji hautoshelezi mahitaji kulingana na idadi ya watu katika eneo hilo la Mji Mdogo wa Mwandiga.

“Waziri wa Maji atatakiwa kuja huku haraka afanyie kazi suala hili. Akifika huku Kigoma apite hapa Mwandiga pia kuangalia ufumbuzi wa suala hili la mtandao wa maji maeneo haya ili tumalize hii changamoto huku Kigoma Kaskazini,” amesema.

Akiwa Wilaya ya Kibondo, Dk Nchimbi amemtaka Waziri Bashungwa kuhakikisha wanalipa fidia ya Sh1.4 bilioni kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kibondo – Mabamba.

Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Kibondo, Dk Nchimbi alipokea kero za wananchi kutoka kwa Mbunge wa Muhambwe (CCM), Dk Florence Samizi ambaye amezungumzia changamoto ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara, Sh1.4 bilioni.

Dk Samizi amezungumzia pia kusimama kwa ujenzi wa Barabara ya Kibondo Townlink kwa sababu mkandarasi aliyepewa kazi hizo hajalipwa fedha zake, jambo lililomfanya asitishe shughuli zake akisubiri kulipwa.

“Ndugu Katibu Mkuu, miradi hii ni muhimu sana kwetu, tunaomba mkandarasi alipwe fedha zake ili akamilishe ujenzi huo kwa wakati ili wananchi waendelee kufurahia miundombinu hiyo,” amesema mbunge huyo wa Muhambwe.

Akizungumza kwenye mkutano wake wilayani Kibondo, Dk Nchimbi ameielekeza Serikali kulipa fidia hiyo ya Sh1.4 bilioni kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kibondo – Mabamba yenye thamani ya Sh60 bilioni.

“Serikali ihakikishe inalipa fedha hizi ili wananchi wapate stahiki zao. Naamini hizi siyo fedha nyingi za kumshinda Waziri Bashungwa kuzilipa kwa haraka haraka,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza.

Vilevile, Katibu Mkuu wa CCM ameitaka Barabara ya Kasulu – Kibondo pia ipewe kipaumbele ili ujenzi wake ukamilike na wananchi waendelee kufanya shughuli zao za usafiri na usafirishaji kwa urahisi zaidi.

Wakati huohuo, Dk Nchimbi amemwelekeza waziri huyo kumlipa mkandarasi anayejenga barabara ya Kibondo Townlink ili aendelee na kazi kwa kuwa, amesimamisha shughuli zake kwa sababu hajalipwa fedha zake.

Pia, amewapongeza mawaziri hao aliowapatia maelekezo kuwa ni watu wachapakazi, wanaojua mahitaji ya wananchi na kutekeleza vizuri ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

Mbunge wa zamani ajiunga CCM

Kigoma ni ngome ya upinzani, ziara ya Katibu Mkuu wa CCM inaendelea kuvunjwa ngome hiyo kwa kuwashawishi makada wa upinzani kujiunga na chama hicho tawala na miongoni mwa waliojiunga ni waliokuwa viongozi wakubwa wa upinzani.

Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa ambayo majimbo na kata zake zimekuwa zikiongozwa na wabunge wa upinzani kutoka vyama vya ACT-Wazalendo, Chadema na NCCR-Mageuzi.

Katika mkutano uliofanyika Kigoma mjini, mbunge wa zamani wa Chadema (Viti Maalumu), Sabrina Sungura ametangaza kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuridhishwa na kasi ya maendeleo katika mkoa huo wa pembezoni.

Mbunge huyo wa zamani aliambatana na wanachama wengine 200 wa vyama vya upinzani waliojiunga na CCM, akiwamo diwani wa Kwakizega kupitia Chama cha DP, Patrick Munisi.

Wanachama hao wa upinzani walijiunga kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi uliofanyika Agosti 4, 2024 Kigoma mjini na kuhudhuriwa na mamia ya wanachama wa chama hicho.

Sabrina alikuwa mbunge wa Chadema, viti maalumu Mkoa wa Kigoma kati ya mwaka 2010 – 2015, sasa amejiunga na CCM akiahidi kwenda kuongeza nguvu katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Tangu Dk Nchimbi alipoanza ziara zake baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Januari 2024, ametembelea mikoa 13 na amepokea zaidi ya wanachama wapya 5,000 kutoka upinzani.

Miongoni mwa mikoa hiyo ni; Songwe, Mbeya, Katavi, Rukwa, Manyara, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Singida na

Akizungumza kwenye mkutano huo, Sabrina amesema ameamua kujiunga na CCM baada ya kutafakari na kutambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesema moja ya sababu iliyomfanya ajiunge na CCM, ni ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa mkoa huo umekuwa ukiteseka na miundombinu ya barabara, lakini sasa Rais Samia ameufungua mkoa huo kupitia miradi mbalimbali ya barabara iliyotekelezwa na inayoendelea kujengwa mkoani humo.

“Nikiwa na akili timamu, bila kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua kujiunga na CCM, sababu kubwa zilizonishawishi kufanya uamuzi huo ni sera za Rais Samia za kutuletea maendeleo wananchi wa Kigoma.

“Wananchi wa Kigoma tumekuwa tukiteseka sana na barabara, nakumbuka nilipokuwa bungeni, tulikuwa na swali moja tu, ni lini wananchi wa Kigoma tutaunganishwa na Tanzania? Sasa tunaona barabara nyingi zimejengwa na Rais Samia ameufungua Mkoa wa Kigoma,” amesema.

Ameongeza kuwa mkoa huo ulikuwa na kero nyingi lakini kupitia R4 za Rais Samia, kero hizo zimetatuliwa ikiwamo kupitia mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Lwiche kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Kwa upande wake, aliyekuwa diwani wa Kwakizega, Patrick Munisi amesema ameamua kujiunga na CCM kwa sababu ameona ajenda zake za kuwaletea maendeleo wananchi zinatekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia.

“Tunajenga nyumba moja kwanini tugombanie fito? Nimeamua kujiunga na CCM ili nikaisaidie Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Hatutakiwi kutofautiana kwenye suala la maendeleo,” amesema diwani huyo wa zamani.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu, Dk Nchimbi amewapongeza wanachama wa upinzani waliojiunga na chama hicho na kuwaahidi ushirikiano katika kutekeleza shughuli za chama hicho.

“Ni haki ya raia kujiunga na chama chochote cha siasa. Nataka niwahakikishie kwamba chama chetu kimewapokea kwa moyo wote na watapata haki zote kama wanachama na tutashirikiana nao kwa kila jambo,” alisema Dk Nchimbi.

Naye Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amemwelekeza Katibu wa CCM Wilaya ya Kigoma kuwakabidhi wanachama hao kadi mpya za CCM ili watambulike kama wanachama halali wa chama hicho tawala.

Wakizungumza na Mwananchi kwenye mikutano ya kiongozi huyo wa chama, wananchi wameeleza kuridhishwa na miradi ya maendeleo inayopelekwa mkoani kwao Kigoma, hata hivyo wameitaka Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ili mkoa huo ufanane na mingine.

Mkazi wa Kakonko, Samuel Chaza amesema barabara ndiyo kero kubwa kwa wananchi wa Kigoma hasa Kibondo na Kakonko, hivyo ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi ulioanza ili kuufungua mkoa huo.

“Tunaomba Serikali ikamilishe hizi barabara katika vipande vilivyobaki. Tunataka mkoa wetu uwe kama mingine huko, tunamshukuru mama Samia kwa kutukumbuka watu wa Kigoma,” amesema mkazi huyo wa Kakonko.

Kwa upande wake, Jesca Bukani amesema wanakabiliwa na changamoto ya maji kwa kuwa wanahangaika kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kila siku, hivyo wameiomba Serikali iwasogezee huduma hiyo kwa haraka.

“Kibondo tunataka maji, hapa kuna shida kubwa ya maji, tunaomba Serikali ituletee maji,” amesema mwanamke huyo huku akielezea kwamba wamekuwa wakitumia maji ya visima ambayo si salama kwa afya zao.

Related Posts