MAKOCHA wa Yanga na Simba, Miguel Gamond na Fadlu Davids ni kama wamenyoosha upanga juu ishara ya kuwa tayari kwa vita ya Ngao ya Jamii hapo kesho Alhamisi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa kila mmoja kueleza alivyojipanga kukabiliana na mwenzake katika mchezo huo wa Dabi ya Kariakoo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa makocha hao kukutana huku ikiwa ni mara ya pili kwa vigogo hao wa soka la Tanzania kuonyeshana ubabe katika mfumo mpya wa uchezaji wa michezo ya ufunguzi wa Ligi, mwaka jana Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti jijini Tanga.
Katika mkutano wa waandishi wa habari ambao ulifanyika leo, Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa, kocha wa Yanga, Gamondi alikumbushiwa matokeo ya Ngao ya Jamii msimu uliopita na kusema hayana nafasi kwake maana huu ni mchezo mpya.
“Mechi zilizopita kwangu hazina nafasi kuelekea mchezo ujao kwa sababu huu ni mchezo mpya, hatujui sana kuhusu Simba, jambo muhimu ilikuwa ni sisi kujiandaa na sio kuwafuatilia,naweza kusema tumefanya hilo kwa zaidi ya asilimia 75,” Gamondi amesema na kuongeza;
“Tupo tayari kwa ajili ya kukabiliana nao,siku zote nimekuwa nikitoa heshima kwa wapinzani wangu, najua kuwa Simba inawachezaji wapya na benchi jipya la ufundi hivyo watakuwa hali mpya kwa hiyo itakuwa mechi ngumu sana na naweza kuiweka katika mzani wa 50/50.
“Kikawaida ni ngumu kujua nini kinaweza kutokea, kesho ni mchezo wa mashindano hivyo utawakuwa mchezo mgumu, naamini utakuwa mchezo mzuri na wa ushindani lakini mpango wangu ni kupata ushindi kwenye mchezo huo, ni kweli kwamba kwenye mchezo uliopita (dhidi ya Red Arrow) tulipoteza sana nafasi hivyo tumekuwa kazi ya kufanya msahihisho.”
Kwa upande wa Fadlu amesema anaamini wanaweza kufanya vizuri katika mchezo huo licha ya mradi wa kuijenga Simba tishio kuwa na wiki tatu lakini kwake sio kikwazo maana anauchukulia mtanange huo kama ilivyo mengine waliyocheza.
“Huu mchezo utaonyesha ni namna gani huu msimu utakuwa baada ya kuwa na wiki tatu kuanza kwa projekti. Nauchukulia huu mchezo kama ilivyo mengine, tutaingia na mpango wa kusaka matokeo ya ushindi,” amesema kocha huyo kutoka Sauzi na kuongeza;
“Yanga ni timu nzuri na tumewaona wana namna tofauti ya uchezaji lakini tunawachezaji wenye vipaji sana, wapo wenye uwezo wa kucheza uwezo wa katika nafasi tofauti, wapo wenye uwezo wa kukaa na mipira, ni suala la kujenga tu kikosi na kuamini Katika lile ambalo tutakuwa tukilifanyaa. Kiukweli mashabiki wategemee tu mazuri.”
Msimu uliopita Simba ilitwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga katika fainali kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya dakika 90 za mchezo huo kutoka suluhu.
Mshindi wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Simba atacheza na mshindi wa mechi ya nusu fainali nyingine inayopigwa pia kesho kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanziba kati ya Azam na Coastal Union.