Heroes Queens yabeba watatu Ligi Kuu

TIMU mpya ya New Heroes Queens inayotarajiwa kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) msimu ujao ipo katika hatua za mwisho kumalizana na Juma Pondamali ili akawe kocha wa makipa.

Awali, Yanga Princess ilikuwa timu ya kwanza kumfuata kocha huyo aliyewahi kucheza Yanga na kuifundishia  makipa, lakini ni kama dili limegeuka.

Diana Mnally

Chanzo cha Mwanaspoti kimeiambia kuwa kocha huyo amekamilisha taratibu zote na kilichobaki ni kusaini nyaraka za mkataba wa miaka miwili.

“Bado kuna vitu kidogo tu havijakamilika, lakini kwa asilimia kubwa tayari. Tumemuona ni kocha anayeifahamu ligi vizuri, ingawa awali hakuwahi kufundisha wanawake, lakini kwa uzoefu wake naamini atatusaidia,” kilisema chanzo hicho.

Anita Adongo

Nje na kocha huyo, pia timu hiyo inatajwa kuwawinda wachezaji watatu wa WPL ambao ni Aisha Mnunka, Diana Mnally (Simba Queens) na beki wa Alliance Girls, Mkenya Anita Adongo.

“Siwezi kuwataja ni wachezaji gani (wanaowawinda), lakini jueni kwamba kuna wachezaji walioachwa Simba, Yanga ambao ni wazuri tutawasajili. Nje na hapo pia watakuja wa kimataifa.”

Lakini mmoja wa wachezaji hao ameliambia Mwanaspoti kuwa tayari ameshatumiwa mkataba na timu hiyo akiuelezea kuwa na maslahi mazuri na pia hauna masharti magumu.

Juhudi za kumpata Pondamali kuzungumzia dili hilo hazikuzaa matunda, kwani hata alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi kuna wakati iliita lakini haikupokewa.

Related Posts