JAJI MWAIMU AIPONGEZA OFISI YA MAKAMU WA RAIS ELIMU YA UDHIBITI TAKA

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma Dodoma leo Agosti 7, 2024. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde na katikati ni Afisa Mazingira, Bw. Abdallah Lungo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bi. Sarah Kibonde akitoa ufafanuzi kuhusu majukumu ya ofisi hiyo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu wakati alipotembelea Banda la Ofisi hiyo katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma leo Agosti 7, 2024.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu akitazama nyaraka mbalimbali zinazoeleza majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakati alipotembelea Banda la Ofisi hiyo katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma leo Agosti 7, 2024.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu akipokea nyaraka mbalimbali zinazoelezea majukumu majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi hiyo, Bi. Sarah mara baada ya kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma leo Agosti 7, 2024.

(NA MPIGAPICHA WETU)

………

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu aipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utoaji wa elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka ambao ni fursa ya ajira.

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo Jumatano Julai 7, 2024) wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa taka zinazozalishwa nchini kwa sasa zimekuwa ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.

“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu kuhusu fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira” amesema Mhe. Jaji Mwaimu.

Aidha Jaji Mwaimu amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais na kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya uhifadhi wa mazingira kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa taka ni fursa iliyojificha na hivyo elimu kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani sio kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.

“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na namna zinavyotakiwa kutenganishwa” amesema Jaji Mwaimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde amesema Ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya habari.

Ameongeza kuwa katika kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa buluu, fursa zitokanazo na taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Kupitia maonesho tuna nyaraka mbalimbali ambazo ni vitabu ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), vipeperushi, majarida ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau nk” amesema Kibonde.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki maonesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2024.

Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.

Related Posts