Kamanda Muliro: Tupo hatua za mwisho za uchunguzi ‘waliotumwa na afande’

Dar es Salaam. Jeshi Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema upelelezi wa tukio la binti anayedaiwa kubakwa na kulawitiwa kisha video yake ikasambazwa katika mitandao ya kijamii upo hatua za mwisho.

Sambamba na hilo, jeshi hilo limekanusha taarifa ilizodai za uzushi kuhusu kifo cha binti aliyefanyiwa ukatili huo, likidai yupo hai.

Video za binti huyo akifanyiwa ukatili huo zilisambaa Agosti 4, 2024 katika mitandao ya kijamii, akionekana na vijana watano waliomfanyia vitendo hivyo.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alithibitisha kukamatwa kwa waliohusika na ukatili huo, huku Jeshi la Polisi ngazi ya Taifa likieleza kuwa katika hatua nzuri za kiuchunguzi.

Taarifa za hatua iliyofikiwa ya kiuchunguzi imeelezwa leo, Jumatano Agosti 7, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Amesisitiza upelelezi kuhusu tukio hilo upo katika hatua za mwisho na hivi karibuni Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime atalitolea ufafanuzi.

“Tupo kwenye hatua ya mwisho hivi karibuni Msemaji wa Jeshi la Polisi atalitolea taarifa,” amesema Muliro wakati akionya taarifa za uzushi kwa kile alichoeleza zinaingilia uchunguzi wa polisi.

Katika hatua nyingine, ametangaza kumshikilia Amos Rwiza (54), Mkazi wa Tegeta kwa kosa la kusambaza taarifa hizo za uzushi juu ya kifo cha binti huyo.

“Tumemkamata mtuhumiwa kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo na ameingilia masuala ya kiuchunguzi,” amesema.

Murilo amesema jeshi hilo linafuata Katiba ya nchi na si kwamba linakataa watu kutoa maoni, isipokuwa linakerwa na upotoshaji huku likiahidi kuendelea kuchukua hatua za kisheria.

Kuhusu mtuhumiwa aliyekamatwa, amesema alileta taharuki kwenye jamii, baada ya kusambaza taarifa hizo za uongo.

Ametoa wito kwa jamii inapobaini kuna vitendo viovu vinafanyika watoe taarifa ili zifanyiwe kazi.

Related Posts