Matampi, Coastal ngoma bado mbichi

SAKATA la kipa Mkongomani, Ley Matampi na Coastal Union, limeendelea kuchukua sura mpya baada ya nyota huyo hadi sasa kutojiunga na kikosi hicho kilichopo visiwani Zanzibar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal Union, Abbas Elsabri amesema, Matampi anaweza kukosekana katika mchezo wa kesho wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, dhidi ya Azam FC kutokana na kutoripoti kambini kwa wakati kama wenzake.

“Matampi alichelewa kujiunga na wenzake na kwa sasa bado yupo jijini Tanga, hivyo kuna uwezekano akaikosa mechi na Azam FC, ila kuanzia hapo tutamuona uwanjani,” amesema Elsabri na kuongeza;

“Matampi bado ni mchezaji wetu halali kwa sababu ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi, hayo mengine yanayozungumzwa ni mitizamo mbalimbali ya watu ambao huwezi kuwazuia kuongea kutokana na kutoujua ukweli ulivyo.”

Wakati Elsabri akizungumza hayo, ila Mwanaspoti linatambua, nyota huyo amekuwa na mgogoro wa kimkataba na klabu hiyo ambayo inadai ilimsainisha mkataba wa miaka miwili huku mwenyewe akidai alisaini mmoja.

Hata hivyo taarifa zinaeleza, Matampi yupo katika mazungumzo na kigogo mmoja wa timu hiyo ambaye anamshawishi aendelee kubakia msimu ujao kwa ajili ya michuano mbalimbali hasa ya kimataifa ambayo nyota huyo ni mzoefu.

Kigogo huyo anapambana ili Matampi aiwahi pia mechi na Azam, ingawa kocha wa timu hiyo, David Ouma inaelezwa amemtoa katika programu za nyota watakaocheza mchezo huo wa kesho, kwani aliwasili nchini tangu Julai 23, mwaka huu ila hakuanza mazoezi na wenzake.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa nyota huyo yupo jijini Dar es Salaam na kigogo mmoja na muda wowote kuanzia sasa atajiunga na timu hiyo Zanzibar, licha ya Ouma kutotaka kumtumia katika mchezo wa kesho.

Nyota huyo alijiunga na Coastal Union msimu uliopita akitokea, Jeunesse Sportive Groupe Bazano huku akichezea timu mbalimbali zikiwemo, TP Mazembe, FC Lupopo na DC Motema Pembe.

Matampi alionyesha kiwango kizuri akiwa na Coastal Union ambapo alitwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, huku akikisaidia kikosi hicho kumaliza nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu kiliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1989.

Related Posts