Babati. Mikataba 17 ya ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) mkoani Manyara, imetiwa saini tayari kwa kuanza ujenzi wake.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika leo Jumatano Agosti 7, 2024, mjini Babati, ikishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.
Mikataba hiyo, yenye thamani ya Sh5.2 bilioniĀ inahusisha ujenzi wa barabara na madaraja katika wilaya tano za mkoa huo.
Makandarasi wote walioshinda kandarasi hizo ni wazawa, jambo lililopongezwa na mkuu huyo wa mkoa.
Hata hivyo, Sendiga amewataka makandarasi hao kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na thamani halisi ya fedha, huku akisisitiza kuwa hatarajii kuona uongezaji wa muda wa utekelezaji wa mikataba hiyo.
Amesema Serikali ina fedha za kutosha na itawalipa makandarasi kwa wakati pindi watakapomaliza kazi na kuwasilisha hati za madai.
Meneja wa Tarura Mkoa wa Manyara, Salim Bwaya amesema makandarasi wameahidi kukamilisha kazi zao kwa wakati na Tarura itahakikisha inawapa ushirikiano wa kutosha ili zikamilike kwa mujibu wa mikataba.
Mikataba hiyo itatekelezwa katika wilaya za Babati, Simanjiro, Kiteto, Hanang na Mbulu.
Mkazi wa Mtaa wa Mruki, Mjini Babati, Chris Bombo amepongeza hatua hiyo na kusema ana matumaini barabara zilizoharibika zitatengenezwa kupitia mikataba hiyo, hasa baada ya mvua kubwa zilizoharibu miundombinu na kukata mawasiliano.