KOCHA Mkuu wa Coastal Union Mkenya, David Ouma amesema anaiheshimu Azam FC kutokana na ubora wa wachezaji ilionao, huku akitoa tahadhari kwa nyota wa kikosi hicho.
Ouma amezungumza hayo wakati timu hizo zikitarajia kupambana kesho katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii utakaopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
“Tunahitaji kufanya kila kitu kilichokuwa bora ili tupate matokeo mazuri, Azam ni timu nzuri yenye wachezaji wenye uwezo wa kuamua mechi, hivyo kwetu ni kipimo kizuri pia kwa sababu tumepata michezo mingi ya kirafiki ambayo imetujengea hali ya kujiamini zaidi,” amesema Ouma.
Ouma aliongeza, katika mchezo huo kuna uwezekano mkubwa akamkosa beki mpya wa kati wa kikosi hicho, Luis Anguti aliyetokea KCCA ya Uganda kutokana na kupata majeraha ya misuli ya paja katika mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
“Tofauti na Anguti ambaye tutamfanyia tathimini ya mwisho kesho kabla ya mchezo, mwingine anayeweza kukosekana ni kipa, Ley Matampi ila waliobaki wote wako katika hali nzuri ya kiafya na utimamu wa kimwili na kiakili,” amesema Ouma.
Timu hizo mara ya mwisho zilikutana Mei 18, mwaka huu ambapo Azam ilishinda mabao 3-0, katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mabao ya Azam katika mchezo huo, yalifungwa na nyota wa zamani wa Coastal Union, Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambaye alifunga mawili huku bao lingine likifungwa na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Mshindi wa mechi hiyo ya kesho atatinga fainali na kukutana na mshindi wa mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga zitakazopepetuana kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.