Serikali ya Uingereza imesema takriban polisi 6,000 wa kupambana na fujo wamewekwa tayari kukabiliana na vurugu ambazo hazijawahi kushuhudiwa nchini humo ndani ya muongo mmoja uliyopita. Mamia ya watu wamekamatwa huku wengine zaidi ya 100 wakishitakiwa. Kulingana na ujumbe ulioonekana katika ukurasa wa Telegram, makundi ya mrengo mkali wa kulia yamepanga maandamano katika maeneo takriban 30 nchini Uingereza na kulenga sehemu zionazowahifadhi wakimbizi.
Vurugu hizo zilitokea baada ya wasichana watatu wenye umri wa miaka tisa, saba na sita kuuwawa na wengine kujeruhiwa vibaya katika tukio la uchomaji visu lililochochewa na taarifa potofu za mtandaoni, juu ya mauaji ya watoto hao eneo la SouthPort, Kaskazini Magharibi mwa Uingereza.
Watu takribani 400 watiwa mbaroni katika ghasia za Uingereza
Baada ya tukio hilo habari za uongo zilisambaa mitandaoni kwamba mshambuliaji alikuwa muomba hifadhi wa kiislamu na mara moja misikiti ikaanza kushambuliwa na vurugu kuanza nchini Uingereza na Ireland ya Kaskazini. Baadae mshukiwa alitambuliwa kama Axel Rudakubana kijana wa miaka 17 aliyezaliwa na kukulia nchini Uingereza na vyombo vya habari vya nchini humo kuripoti kwamba wazazi wake wanatokea Rwanda.
Starmer asema anapambana kuhakikisha Uingereza ni salama
Hata hivyo, onyo kali tayari limeshatolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliyesema yoyote atakayehusika na vurugu hizo au kuchochea ghasia za aina yoyote mitandaoni atakabiliwa na mkono wa sheria.
Vurugu katika miji mingine Uingereza yamewaonyesha waandamanaji wakiwarushia mawe polisi, kuchoma moto magari na kushambulia misikiti na hoteli mbili zinazokaliwa na waomba hifadhi. Serikali mpya ya Uingereza iliyoingia madarakani mwezi Julai inapambana na mgogoro wake wa kwanza mkubwa. Starmer amesema wanapambana kuhakikisha kila mtu nchini Uingereza anajiskia yuko salama.
“Jukumu letu la kwanza lazima iwe jamii zetu, kuziweka salama. Hiki ndicho kipaumbele changu. Polisi wanafanya kazi ngu katika mazingira magumu na nadhani kila mtu anapaswa kuungwa mkono katika kuhakikisha mitaa yetu ipo salama, jamii zetu zipo salama na thabiti.” aliongeza kusema Keir Starmer Waziri Mkuu wa Uingereza.
Starmer kuunda ‘jeshi la dharura’ kukabiliana na vurugu
Kwa upande wake Meya wa Mji wa London Sadiq Khan aliandika katika ukurasa wake wa X, kwamba serikali ya Starmer imeweka mikakati mipya ya kuhakikisha maeneo ya kuabudu inayolengwa inalindwa. Amesema matukio ya kushtusha ya kuogopesha yanayoendelea nchini humo yamewaacha waislamu na makundi ya wachache kuwa na hofu huku akiwahimiza raia kujuliana hali na kuhakikisha kila mmoja yuko salama. Khan amesema Uingereza haitovumilia visa vya kibaguzi, chuki dhidi ya waislamu na chuki dhidi ya wayahudi au aina yoyote ile ya chuki.
Chanzo: ap, afp, reuters