Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema mradi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi una umuhimu wa kipekee, akiwapongeza wadau wote waliofanikisha kuukalimisha na kuanza uzalishaji wake Julai mosi, 2024.
Mkuu huyo wa nchi, amesema kiwanda hicho cha Kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), kina wanahisa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la la Magereza kupitia Shirika la Uzalishaji Mali (Shima).
Rais Samia ametoa kauli hiyo, leo Jumatano, Agosti 7, 2024 wakati akizindua kiwanda hicho, kilichopo eneo la Mbigiri wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku sita.
Amesema kukitokea mabadiliko ya sera na kodi au yoyote lazima kiwanda hicho kizalishe kwa ajili ya nchi, akisema huo ndiyo umuhimu wa Kiwanda cha Mkulazi, huku akiahidi Serikali kufanya kila linalowezekana ili kuongeza wigo wa kiwanda hicho.
“Mashirika ya Serikali yamejenga kiwanda hiki, sasa umuhimu wake upo wapi? Serikali inapofanya kazi kuna mabadiliko ya sera na kodi ambayo huenda sekta binafsi wasiridhike nayo na kuanza kurudi nyuma kidogo na kupunguza uzalishaji.
“Toka nimeingia Morogoro nimeshughulika na viwanda viwili vya sukari vya Mtibwa, Kilombero (sekta binafsi) na Mkulazi ni cha tatu. Vile viwili vya sekta binafsi, lakini hiki cha Mkulazi kina umuhimu wake kwa sababu kinamilikiwa na taasisi za Serikali,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia amesema Serikali inafanya kila jitihada za kusogeza sekta binafsi kufanya kazi na Serikali ikiwamo kuwekeza ndani ya nchi na kufanya miradi kwa pamoja.