Safari kina Mdee kurejea Chadema yaiva

Dar es Salaam. Kuna vuguvugu la chinichini la baadhi ya wabunge wa viti maalumu kati ya 19 waliovuliwa uanachama wa Chadema kurejea ndani ya chama hicho.

Vuguvugu hilo ambalo pia linazua mjadala wa pande mbili, liliwekwa wazi Agosti 6, 2024 kupitia kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu kuwa “CCM itamuota sana Mdee juu ya kuhamia katika chama hicho.”

Mkakati huo unaowahusisha baadhi ya viongozi wa Chadema na wabunge wachache wa kundi hilo, umekuwa unakwenda kichinichini na sasa umeshika kasi kipindi hiki ambacho Tanzania inakaribia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.

Wabunge hao ni wale ambao Novemba 27, 2020 Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uanachama kutokana na uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu ilhali msimamo wa chama hicho ulikuwa ni kususia matokeo yote ya uchaguzi mkuu na matokeo yake, zikiwemo nafasi hizo.

Wakati chama hicho hakijakaa kuwateua wabunge hao, kundi hilo liliibuka bungeni na kuapishwa na kuwa wabunge.

Wabunge hao ni Halima Mdee, Ester Bulaya, Esther Matiko, Sophia Mwakagenda, Salome Makamba, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa na Hawa Mwaifunga.

Wengine ni Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest na Conchesta Rwamulaza.

Taarifa ambazo Mwananchi linazo si wabunge wote 19 walioianza safari ya kurudi Chadema, bali ni wachache na hata hivyo, uamuzi wa kurejea kwao unawagawa vigogo ndani ya chama hicho.

Wakati hali ikiwa hivyo, wapo ambao kwa matendo yao wanaonyesha kila dalili za kuhamia CCM na wameanza kusaka nafasi katika majimbo mbalimbali, ikiwemo mikoa ya Singida na Shinyanga.

Akitoa salamu za Chadema kwenye mazishi ya mama mzazi wa Halima Mdee, Theresia, yaliyofanyika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Mwalimu alidokeza hilo kwa kauli ambayo imeibua mjadala kwenye makundi ya Chadema.

“Baba Paroko kuna jambo limechokozwa, lakini limeshajibiwa, eti (Mdee) anafanana na huko? (aliuliza Mwalimu na kujibiwa “hapana” na waombolezaji, kisha akaendelea..) hafanani ee… basi watamuota sana,” alisema.

Mwalimu alitoa kauli hiyo akijibu kilichozungumzwa awali na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu aliyemkaribisha Mdee ndani ya chama hicho tawala.

 “Sasa dadaangu Halima kwa sababu huko kwingine hakueleweki, njoo huku (CCM),” alisema.

Kauli yake ya Mwalimu kuwa wanaomtaka ahamie CCM watamuota sana, inaibua swali la je, amejuaje kama uamuzi huo kwa Mdee utabaki ndoto? Hata hivyo, Mwalimu alipotafutwa na Mwananchi afafanua kauli yake Agosti 7, 2024, amesema hilo lilikuwa jambo la msibani na liliishia huko.

“Tulichokifanya ni kwamba CCM walituchokoza na sisi ikabidi tuwajibu, lakini yaliyotokea msibani yaishie palepale. Tungetaka yatoke nje tungeyazungumze nje,” amesema.

Amesisitiza kuwa hakulenga kutafsiri chochote, na hivyo itafsiriwe kuwa ni kauli ya msibani na iishie kwenye msiba. Agosti 5, 2024, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alikuwa sehemu ya waombolezaji waliofika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kibangu, Dar es Salaam kuaga mwili wa marehemu kabla ya kusafirishwa kwenda Kilimanjaro.

Katika maelezo yake, Mbowe alisema: “Mimi binafsi na wenzangu katika harakati tulimwona mama Halima Mdee kama mlezi wa harakati na kama mtunzi wa imani yetu ya kuitafuta haki katika Taifa, tulimwona kama mama mlezi aliyetuzalia viongozi walio bora sana kwa wakati wote.”

Vyanzo mbalimbali ndani ya Chadema vimelieleza Mwananchi kuwa kauli ya Mwalimu haikuwa ya bahati mbaya.

Kimoja kati ya vyanzo hivyo, kimesema alichokisema Mwalimu kinalenga kuwaandaa wanachama kuhusu kurejea kwa kina Mdee na baadhi ya wenzake.

Kilieleza kuwa kuna jitihada kubwa zinafanyika za kuhakikisha kina Mdee na wenzake akiwamo Bulaya wanarejea kundini, ingawa si wote watakaorejea kwa sababu wengine wameshaonyesha nia ya kwenda CCM,” amesema.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia hilo, Bulaya amesema yuko msibani hivyo asingeweza kuzungumzia hilo.

“Lakini si unajua nipo msibani ndugu yangu, mimi nipo msibani huku naomba niache kwanza,” alijibu Bulaya baada ya kuulizwa suala hilo.

Mmoja wa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, alipoulizwa amesema: “Katika siasa hakuna adui wala rafiki wa kudumu. Unajua katika hilo kundi la Mdee wapo ambao misimamo yao inaendelea kiupinzanipinzani na wengine wapo ki-CCM.”

Katika hilo anaeleza kuwa baadhi yao (bila kuwataja majina) wamekuwa wakishiriki shughuli zinazowahusisha na CCM na hata bungeni michango yao imekuwa ikijielekeza huko.

“Mdee, Matiko, Bulaya na Mwakagenda kama unafuatilia wameendelea kuwa na misimamo yao, si kama wengine ambao wameelekea CCM wanasubiri wamalize ubunge, kwa hiyo kurudi kwao haitakuwa jambo jipya ndio siasa zilivyo,” amesema.

Kiongozi huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa sababu za kiitifaki, amesema kuna uwezekano wa wanasiasa hao kuandika barua ya kuomba msamaha, kisha kamati kuu itawasamehe na taarifa zake kuwasilishwa katika Baraza Kuu.

“Wanaweza kuandika barua za kuomba msamaha, kisha kamati kuu inawasamehe na wanakuwa wanachama wa kawaida, maisha yanaendelea, lakini ukweli kuna jitihada zinafanyika ili kina Mdee kurejea,” alieleza.

Kiongozi huyo amekwenda mbali akikumbushia hatua ya Mbowe, Mdee na Bulaya kukutana katika harambee ya kuchangia kanisa mkoani Kilimanjaro mwaka 2023, iliyozua maneno ndani ya chama hicho.

Kufuatia hatua hiyo, baadhi ya makada wa chama hicho walihoji Mbowe anapata wapi ujasiri wa kuwaalika kina Mdee walipingana na maamuzi ya chama na kukataa kuomba msamaha.

Harambee hiyo ilifanyika Desemba 31, 2023 ikilenga kufanikisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa kanisa la Betheli kwenye Usharika wa Nshara, Machame ambako Mbowe alishiriki kwa mwaliko wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo.

Lakini, Mbowe, Mdee na Bulaya na kiongozi mmoja wa Chadema wachangie harambee hiyo na wote walishiriki kwa kwenda kanisani na kuchangia.

Chanzo hicho kinaeleza kuwa baada ya viongozi hao kukutana kiliitishwa kikao cha kutafuta suluhu lakini kigogo mmoja wa chama hicho alisusa na kuondoka.

Kuondoka kwake, amesema kulitokana na msimamo wake mkali dhidi ya wabunge hao 19. “Katika chama wenye misimamo mikali kuhusu suala la kina Mdee wapo wawili, ambao hawataki kusikia suala la wabunge 19, lakini ukweli kuna hiyo ‘movie’ inafanywa ili hawa watu warudi katika chama, kauli ya Salum (Mwalimu) siyo bahati mbaya bali ni kimkakati ya kuwaandaa watu,” amesema.

Amesema hali hiyo huenda pia ikajitokea kwenye kikao cha kamati kuu cha siku mbili kitakachoanza Agosti 8, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya uteuzi wa makatibu wa kanda za Nyasa, Victoria, Magharibi na Serengeti zilizomaliza uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.

“Suala la kina Mdee linaweza kuchomoza ndani ya kamati kuu, kama mengineyo lakini siyo ajenda,” amesema.

Askofu akemea kuwabeza Kwenye shughuli ya mazishi ya mama mzazi wa Mdee, Askofu Shoo amesema hafurahishwi na jina wanaloitwa wabunge hao 19 la Covid-19 na kutaka watu waheshimiane bila kujali wamesimama upande gani.

 Amesema tangu mwanzo aliwakemea baadhi ya waliokuwa wakilitamka jina hilo mbele yake na aliwahoji kwa nini wanaitana jina hilo.

“Sasa nikawauliza wanangu mmefikia huko kwa sababu za ushabiki tu, kuchagua majina ambayo hayafai ndiyo mnawaita wenzenu au mnatafuta majina ambayo hayafai ndiyo mnajiita ninyi, nikasema hapana,” amesema Dk Shoo.

Hata hivyo, amesema alichokiona katika maziko hayo ni alama ya upendo, utu katika jambo ambalo linamgusa kila mmoja na wameamua kuweka tofauti zao kando na kuwa huo ndio upendo wa kweli wa Kimungu.

Si ajabu katika siasa Kutokana na vuguvugu hilo, Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema ni vigumu kupima athari na faida za kurejea kwa baadhi ya wanasiasa hao ndani ya Chadema.

Hata hivyo, amesema endapo watarejea litakuwa suala la kawaida kama Chadema ilivyompokea hayati Edward Lowassa akitokea CCM, inashindwaje kuwapokea wanasiasa iliowalea yenyewe.

“Moja, chama cha siasa mtaji wake ni wanachama na wakati wowote unapoona chama kinafukuza wanachama si kwamba kinapenda, ila ni katika kuangalia wale wanaosababisha udhaifu kwenye chama.

 “Inawezekana, dhana ya kawaida katika siasa ukizingatia siasa si uadui, ni ushawishi katika muda fulani na kwa sababu fulani,” ameeleza.

Iwapo watarejea, amesema hakuna kati ya Chadema wala wabunge hao atakayepaswa kuonekana mkosaji.

“Lakini kipindi kile ilikuwa lazima uongozi uchukue hatua ili kuleta utulivu ndani ya chama,” amesema.

Hata hivyo, amesema Mdee na Bulaya ni miongoni mwa wanachama muhimu na Mbowe amewahi kukiri hilo, licha ya kukiuka utaratibu hadi kufukuzwa, na wakiwa nje ya Chadema baadhi yao hawakuwahi kufanya kitu kibaya.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts