Samia afunguka sakata la kupanda bei ya sukari, ‘ilivyomtetemesha’

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesimulia namna sakata la kupanda bei ya sukari lilivyomweka katika wakati mgumu, akisema uwepo wa kiwanda cha Mkulazi utawezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo kuwa wa uhakika.

Rais Samia alieleza hayo jana alipokuwa akizindua kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichojengwa na Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Uzalishaji Mali (Shima), wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Katika maelezo yake, Rais Samia amesema: “Nilipata mtetemeko wa sukari, nadhani ilikuwa Februari, Machi kuelekea Aprili ziliponyesha mvua nyingi, viwanda havikuweza kuzalisha, lakini sukari baadhi ya maeneo ilikuwepo katika maghala watu walibana na hatimaye ikapanda bei kupindukia na kusababisha Watanzania kushindwa kuinunua.

“Sukari siyo chakula chetu wakubwa, bali cha watoto kwa sababu wakubwa kuna umri ukifika tunaanza kuikataa, lakini watoto wanaitumia hata mama lishe matumizi kwao ni makubwa, unapomwambia akanunue Sh7,000 au Sh8,000 kwa kilo haiwezekani,” amesema.

Katika kipindi hicho alichoeleza Rais Samia bei ya sukari ilipanda hadi kufikia kati ya Sh5,000 na Sh7,000 katika baadhi ya maeneo.

Wazalishaji walipopewa vibali vya kuagiza kutoka nje hawakuingiza kwa kiwango kilichokusudiwa.

Kutokana na mazingira hayo, bei ya sukari iliendelea kuwa juu hadi Serikali ilipotoa vibali kwa kampuni nyingine kuagiza bidhaa hiyo. Hata hivyo hatua hiyo ya  Serikali, ilikosolewa na wazalishaji wakidai inaathiri shughuli zao.

Sakata la upatikanaji wa sukari limekuwa likijitokeza mara kwa mara si katika utawala wa Rais Samia hata katika utawala wa awamu ya tano hali hiyo ilijitokeza, ambako msako mkali uliendeshwa ili kuwabaini wanaodaiwa kuificha bidhaa hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa Mkulazi, amesema hata kukitokea mabadiliko ya sera na kodi au yoyote kiwanda hicho hakitarudi nyuma katika uzalishaji kwa manufaa ya Taifa.

“Serikali inapofanya kazi kuna mabadiliko ya sera na kodi ambayo huenda sekta binafsi wasiridhike nayo na kuanza kurudi nyuma kidogo na kupunguza uzalishaji,” amesema.

Rais Samia amesema huo ndiyo umuhimu wa kiwanda cha Mkulazi, akiahidi Serikali kufanya kila linalowezekana ili kuongeza wigo wa kiwanda hicho.

Alisisitiza umuhimu wa Mkulazi akisema hata kukitokea changamoto ya mvua nyingi  kiwanda hicho kitatoa akiba yake na kuipeleka sokoni kwa ajili ya Watanzania kupata bidhaa hiyo kwa urahisi.

“Tutakwenda kuikwangua akiba yote itoke kwenye ghala na kuipeleka kwa wananchi bila migogoro na heshima itakuwepo, lakini kwa mtu binafsi huwezi kumuingilia katika ghala lake na kumlazimisha atoe, labda uende na bunduki lakini katika utawala bora hilo halipo, labda kuwepo kwa dharura,” amesema.

Rais Samia alimuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, kuanza mchakato wa kushirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la Mkulazi namba mbili.

Amesema hatua hiyo ikifanikiwa, itawezesha upatikanaji wa uhakika wa sukari nchini, ndiyo maana Serikali iliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kurekebisha kanuni itakayowezesha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula.

“Huko mbele tutaifanya NFRA kununua sukari na kuhifadhi ili inapotokea uhaba wa chakula kiwandani (Mkulazi) na NFRA ipo tunakwenda kuwahudumia Watanzania bila kuwepo na changamoto kubwa,” amesema.

Mbali na hilo, Rais Samia alitaka uendelevu wa kiwanda hicho, akisema uzoefu unaonyesha vitu vinavyomilikiwa na Serikali uangalizi wake unakuwa tofauti na sekta binafsi. Aliutaka uongozi wa Mkulazi kuwa imara katika uendeleshaji wa mradi huo ili kuwepo na uendelevu.

“Mradi ukifa na wewe umekufa (meneja mradi), vinginevyo ukiishi basi na mradi huu uishi. Nawaona wenzako wanacheka, mradi huu uishi kama kufa hautakufa peke yako pia, msaidieni ili mradi uwe endelevu kwa manufaa ya Taifa,” ameagiza Rais Samia.

Awali, uongozi wa Kampuni ya Hodhi ya Mkulazi (MHCL) ulieleza kiwanda hicho kimejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu, kina uwezo wa kuchakata miwa tani 500,000 sawa na uzalishaji wa tani 50,000 kwa mwaka.

“Uzalishaji wa sukari kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ulianza Julai mosi mwaka huu, kwa tani 200 hadi 250 kwa siku,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya MHCL, Dk Hildelitha Msita.

Dk Msita amesema sukari ya Mkulazi kwa sasa inapatikana sokoni ikijulikana kama ‘mafao sugar utamu kama wote.’

Amesema MHCL ina mpango wa kuongeza wigo wa kuzalisha bidhaa zitokanazo na miwa ikiwemo ethano itakayotumika kama malighafi ya kutengeneza dawa.

“Hatua hii itawezesha kampuni kuongeza mapato na kushusha bei ya sukari, lakini tunaomba Serikali iendelee kutoa fedha ili kuwezesha ujenzi wa barabara katika mashamba ya miwa ya wakulima wadogo,” amesema Dk Msita.

Kwa mujibu wa Dk Msita, wanahisa wakubwa wa MHCL ni NSSF na Jeshi la Magereza kupitia Shima.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema watafanya kila jitihada kuhakikisha wanakilinda kiwanda cha sukari cha Mkulazi kitakachozalisha sukari ya viwandani pia.

Bashe amesema Bodi ya Sukari Tanzania imeanza utaratibu wa kupitia kanuni za namna ya kukilinda kiwanda hicho, ambacho kitawezesha kupunguza tani 50,000 za sukari za viwandani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

“Niwape moyo watu wa Mkulazi hii bidhaa itaingia sokoni kwa uwezo wa Mungu siyo muda mrefu, kabla ya Juni mwaka 2025 kanuni zitakuwa zimebadilishwa ili kukilinda kiwanda hiki kinachozalisha sukari ya viwandani pia,” amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema Rais Samia anaendelea kuweka historia ya kuongeza viwanda katika utawala wake hasa katika sekta ya sukari ambayo imekuwa na changamoto kubwa.

“Sasa unakwenda kuweka historia, chini ya sera zake Kilombero Sugar itazalisha tani 271,000, Kagera tani 155,000, hapa tani 50,000 na Bagamoyo Sugar tani 35,000. Ndani ya muda mfupi zaidi tunakwenda kukidhi matakwa ya matumizi ya sukari,” amesema Dk Jafo.

Agosti 3, katika uzinduzi wa alipozindua bwawa la umwagiliaji la Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa mkoani Morogoro, Waziri Bashe amesema mahitaji ya sukari nchini kwa sasa ni tani 650,000, lakini matarajio ya uzalishaji mwaka huu ni tani 550,000.

Amesema ifikapo mwaka 2026, uzalishaji unatarajiwa kufikia tani 750,000, huku mwaka 2030 ukifika tani milioni moja.

Related Posts