Samia apongezwa kukikwamua Kiwanda cha Sukari Mkulazi

Dar es Salaam. Uongozi wa Kampuni ya Hodhi ya Mkulazi (MHCL) imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuukwamua mradi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi uliokwama kwa sababu mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 7, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi Wakurugenzi ya MHCL, Dk Hildelitha Msita, wakati akitoa salamu za kampuni mbele ya Rais Samia katika uzinduzi wa kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2021, wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

“Tunakushuruku kuridhia kuendelea kwa mradi huu kwa kuwezesha kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda Julai 2021, kama utakumbuka ulipoingia madarakani (Machi 19, 2021) mradi huu, ulikuwa na changamoto nyingi, kwa maono yako uliridhia uendelee.

“Kiwanda hiki kimejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu, kina uwezo wa kuchakata sukari tani 500,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa sukari kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ulianza Julai mosi mwaka huu, kwa tani 200 hadi 250 kwa siku,” amesema Dk Msita.

Dk Msita amemueleza Rais Samia kuwa sukari ya Mkulazi kwa sasa inapatikana sokoni ikijulikana kama ‘mazao sugar’ au ‘tamu kama wote.’ Amesema MHCL ina mpango wa kuongeza wigo wa kuzalisha bidhaa zitokanazo na miwa ikiwamo ethanol itakayotumika kama malighali ya kutengeneza dawa.

“Hatua hii itawezesha kampuni kuongeza mapato na kushusha bei ya sukari, lakini tunaomba Serikali iendelee kutoa fedha ili kuwezesha ujenzi wa barabara katika mashamba ya miwa ya wakulima wadogo,” amesema Dk Msita.

Amesema wanahisa wakubwa wa MHCL ni Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la la Magereza kupitia Shirika la Uzalishaji Mali (Shima).

Katika hatua nyingine, Dk Msita amesema mradi huo umetekelezwa kwa ushiriakino na wadau mbalimbali ukiwamo uongozi wa Mkoa wa Morogoro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Bonde la Mto wa Wami, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Bodi ya Sukari Tanzania na wengine.

Related Posts