Sinwar anapaswa kusimamia amani ya Gaza – DW – 07.08.2024

Yahya Sinwar aliteuliwa siku ya Jumanne kuwa kiongozi mkuu wa kisiasa wa kundi la wanamgambo la Hamas. Sinwar anadaiwa kupanga shambulizi la Oktoba 7 lililofanyika Kusini mwa Israel na kuchochea mgogoro unaoendelea kati ya Israel na kundi hilo mjini Gaza. Sinwar amechukua nafasi ya Ismail Haniyeh aliyeuwawa Julai 31 mjini Tehran katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel.

Mauaji hayo ambayo Iran inainyooshea kidole cha lawama Israel, yamesababisha hofu katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati huku mashambulizi ya kulipiza kisasi yakitarjiwa. Wasiwasi pia umetanda ndani ya kanda hiyo baada ya Israel kumuua kamanda wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon wiki iliyopita.

Hamas yamteua Yahya Sinwar kuchukuwa nafasi ya Haniyeh

Sasa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Blinken amesema kiongozi huyo mpya wa Hamas ana jukumu la kuhakikisha makubaliano ya kusitisha mapigano yanafikiwa kwa lengo la kuleta amani ya Mashariki ya kati. Lakini licha ya kauli hiyo bado kuna wasiwasi wa kuzuka kwa vita zaidi baada ya Israel kukasirishwa na uteuzi huo, kupitia waziri wake wa mambo ya nje Israel Katz, Israel imesema uteuzi huo ni sababu nyengine kuu ya kuendelea kulitokomeza kundi hilo la Hamas kutoka katika uso wa dunia. 

Hamas yasema bado ipo Imara

Yahja Sinwar kiongozi wa Hamas
Hamas imesema uteuzi wa Sinwar unatoa ujumbe mzito kwa Israel kuwa bado ni imara na inaendelea na operesheni zake.Picha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Kwa upande wake Hamas imesema uteuzi wa Sinwar unatoa Ujumbe mzito kwa Israel kwa Hamas bado ni imara na inaendelea na operesheni zake. Washirika wa kundi hilo wanamgambo wa Hezbollah walioko Lebanon wamempongeza Yahya Sinwar wakisema uteuzi huo unathibitisha kuwa adui ameshindwa kufanikisha lengo lake kwa kumuua Haniyeh na maafisa wengine wa Hamas.

Wakati hofu ya machafuko zaidi ikizidi kutanda katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia Hezbollah na Iran kuapa kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh pamoja na Kamanda wao Fuad Shukr.

Uturuki kujiunga kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel

Huku hayo yakiarifiwa rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema amezungumza na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na amemueleza kwamba kama mataifa ya Magharibi yana nia ya kweli ya kusitisha vita, ni lazima wailazimishe Israel kuachana na mauaji la halaiki inayotekeleza Gaza na kuridhia makubaliano ya kusitisha mapigano. Pezeshkian amesema Jamhuri hiyo ya kiislamu kamwe haitokuwa kimya kutakapokuwa na hatua za kichokozi au kitisho cha usalama wake na matakwa yake.

Kwengineko jeshi la Israel limetoa amri mpya kwa wapalestina kuondoka katika maeneo ya Kaskazini mwa Gaza ambayo yalikuwa ya kwanza kulengwa mwanzoni mwa vita vya Israel na Hamas mnamo Oktoba 7.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Chanzo: ap,afp, reuters

Related Posts