Tabora. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ipo katika hatua za mwisho za kununua ndege maalumu itakayogharimu zaidi ya Sh6 bilioni kwa ajili ya kumwaga sumu ili kuua kweleakwelea wanaoshambulia mazao.
Inaelezwa kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza hasara wanazokumbana nazo wakulima kila mwaka kutokana na ndege hao.
Ofisa Kilimo Mkuu kutoka TPHPA, Grace Matiku akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Agosti 7, 2024, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wakulima kupata hasara kubwa kila mwaka kutokana na ndege hao kuifanya Tanzania kuwa makazi yao.
“Serikali iko katika hatua za mwisho za kununua ndege maalumu itakayotumika kuwaangamiza ndege aina ya kweleakwelea na nzige wekundu ambao wamekuwa tishio kwa mazao ya nafaka. Karibia kila mkoa tumekuwa na malalamiko ya uwepo wa ndege hawa, sasa tunachukua hatua zaidi,” amesema Matiku.
Amesema awali, Tanzania ilikuwa ikipata ndege za kudhibiti nzige jangwani kutoka shirika la kimataifa lenye makao yake Ethiopia na Zambia, huku Tanzania ikiwa mwanachama.
Hata hivyo, ujio wa ndege hiyo mpya itakayomilikiwa na Serikali ya Tanzania utaondoa usumbufu uliokuwepo wa kusubiri ndege hizo kutoka mashirika rafiki, jambo ambalo lilichukua siku 5-14 kupata msaada wakati wa changamoto kwa wakulima.
Wakulima wameelezea matumaini yao kuhusu hatua hii mpya. Zabron Joseph, mkazi wa Tabora, amesema ndege hiyo itawasaidia wakulima kuvuna mazao yao bila usumbufu wala uharibifu.
“Tunaipongeza Serikali kwa kuamua kununua ndege hii maalumu ya kupulizia sumu kwa ndege hawa kweleakwelea ambao wanatuingiza hara kila mwaka,” amesema Joseph.
Naye mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Idda Stephano mkazi wa Manispaa ya Tabora amesema mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya ndege hao waharibifu.
“Mimi msimu uliomalizika nililima hekari 2,000 huko Igunga, lakini ndege wakavamia na kula karibu hekari 500, jambo lililonisababishia hasara kubwa,” amesema Stephano.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na TPHPA, kundi la ndege wapatao milioni tano wanapovamia shamba wanaweza kula hadi tani 50 za nafaka, kwa kuwa ndege mmoja ili ashibe anakula takriban gramu 10 za nafaka.