Uamuzi  sakata la uhalali wa katiba ya Yanga wakwama

Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi wa shauri la maombi ya marejeo ya uamuzi uliobatilisha Katiba ya Klabu ya Dar es Salaam, Young African Sports,  maarufu kama Yanga, ya mwaka 2011.

Uamuzi huo ulipangwa kutolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Frank Kiswaga leo Jumatano, Agosti 7, 2024, saa 9:00 Alasiri.

Hata hivyo, Hakimu Kiswaga hakuweza kutoa uamuzi huo na badala yake ameahirisha hadi keshokutwa, Ijumaa, Agosti 92024, saa 4:00 asubuhi.

Wakati akiahirisha utoaji wa uamuzi huo, Hakimu Kiswaga hakutoa sababu yoyote.

Shauri hilo lilipoitwa, Wakili wa wajibu maombi katika shauri hilo, Jacob Mashenene hakuwepo mahakamani.

Hivyo baada ya mawakili wa Yanga, Kalaghe Rashid na Respocius Didace  kujitambulisha, Hakimu  Kiswaga amewauliza wajibu maombi katika shauri hilo, Juma Ally Magoma na Geofrey Mwaipopo, mahali aliko wakili wao.

“Wakili wetu ana shauri lingine Bagamoyo Mheshimiwa, lakini yuko njiani atakuja,” amejibu Magoma.

Baada ya jibu hilo la Magoma ndipo Hakimu Kiswaga akabainisha kuwa hatasoma uamuzi huo leo.

“Hata hivyo, uamuzi wenu nitautoa keshokutwa, Agosti 9, (2024) saa 4:00 asubuhi,” amesema Hakimu Kiswaga.

Katika shauri hilo Klabu ya Yanga iliiomba Mahakama hiyo irejee uamuzi  uliobatilisha Katiba yake ya mwaka 2011.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Pamela Mazengo, Agosti 2, 2023 ilibatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.

Uamuzi huo ulitokana na kesi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na Magoma na mwenzake Mwaipopo,  wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo.

Katika kesi hiyo, Magoma na Mwaipopo walipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.

Hivyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa, Katiba ya mwaka 2011 ni batili na wajumbe wa Bodi waliopo kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.

Kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo kwa madai kuwa walipelekewa wito wa mahakama lakini hawakuitikia.

Katika uamuzi wake mahakama hiyo ilikubaliana na madai na maombi ya kina Magoma, ikatamka kuwa Katiba ya sasa ya Yanga, (2011) haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968.

Hivyo ilisema kuwa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.

Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika ( mwenyekiti ), Fatma Abeid Aman Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.

Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batil.

Hata hivyo, hukumu hiyo haikuwahi kujulikana hadi Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaya ilipoibuka katika vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani hapo kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.

Uongozi wa klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza hakuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo, huku akibainisha kuwa klabu hiyo itavhukua hatua za kuupinga, Kwa kuwa haikukubaliana nao.

Hata hivyo, hadi wakati huo ilipoupata uamuzi huo  ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.

Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga uamuzi huo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.

Shauri hilo lilisikilizwa Jumatatu, Agosti 5, 2024, ambapo Klabu ya Yanga iliwasilishwa na mawakili Rashid na Didace, huku wajibu maombi, Magoma na Mwaipopo waliwakilishwa na Mashenene.

Wakati wa usikilizwaji huo,awakili wa Yanga walibainisha kile wanachokionw kama.kasoro katika hukumu ya awali wanayoipinga.

Hivyo mahakama hiyo katika uamuzi wake itakaoutoa kama itakubaliana na hoja za Yanga basi itatengua uamuzi wake huo wa awali ulipwapa ushindi kina Magoma (uliobatilisha Katiba ya Yanga ya mwaka 202l11).

Lakini kama haitakubaliana na hoja hizo basi italitipilia mbali shauri lao hilo na hivyo hukumu ya awali itasimama, na kina Magoma wanaweza kuendelea na hatua za utekelezaji.

Hata hivyo, upande wowote ambao hautakubaliana na uamuzi huo ikiona kuna haja basi unaweza kuchukua hatua zaidi kama kukata rufaa Mahakama Kuu.

Related Posts