Ripoti ya robo mwaka ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema idadi ya televisheni za mtandaoni nchini imepungua kutoka 231 hadi 215. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wamiliki wa leseni za televisheni za mtandaoni zimepungua kwa asilimia 7.4. Upungufu huo umeshuhudiwa kati ya mwezi Machi hadi Juni 2024.
Kwa sasa, gharama za usajili wa televisheni nchini ni Sh 500,000 kutoka Sh milioni moja, iliyokuwa awali.
Wakati huohuo, TCRA imesema kuwa majaribio ya utapeli kwa njia ya mtandao yameongezeka kwa wastani wa asilimia 57, huku kukiwa na majaribio 22, 257 hadi kufikia mwezi Juni, 2024.
“Mikoa ya Rukwa na Morogoro ndiyo inayoongoza, ikiwa na zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai nchini. Mbeya, Dar es Salaam na Arusha zinafuata kwa majaribio ya ulaghai kwa zaidi ya 1 hadi 10,” imesema TCRA.
Mikoa mingine ya Kaskazini Pemba, Kusini Unguja na Kusini Pemba ina idadi ndogo ya majaribio. Kila mkoa ulirekodi asilimia 0.01.
Kulingana na TCRA, hali ya mawasiliano katika robo inayoishia Juni 2024 imeonesha maendeleo makubwa kwa kuongezeka kwa utumiaji wa huduma za mawasiliano, ikichochewa na ushindani endelevu wa bei za huduma.
Moja ya mafanikio hayo ni kuenea kwa mtandao wa simu za mkononi katika teknolojia mbalimbali, ambapo mtandao wa 3G umeenea kwa asilimia 89 ya watu, na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya Intaneti.