Vital’O yapania kuiondosha Yanga Ligi ya Mabingwa Afrika

MABINGWA wa Ligi Kuu Burundi msimu uliopita Vital’O wamepania kuwaondosha Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mapema pale timu hizo mbili zitakapokutana katika hatua ya awali ya michuano hiyo.

Vital’O na Yanga zitakutana katika mchezo wa kwanza Agosti 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambapo wakali hao wa Burundi watakuwa wenyeji baada ya kuchagua kutumia dimba hilo kutokana na kukosa uwanja wenye vigezo nchini kwao.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kupigwa Agosti 24 mwaka huu ambao Yanga itakuwa mwenyeji kwenye dimba la Benjamin Mkapa na mshindi wa jumla atasonga mbele.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msemaji wa Vital’O, Arsene Bacuti amesema wanajiamini na wako tayari kuchuana na Yanga kisha kuiondosha katika michuano hiyo mikubwa Afrika.

“Tunaenda kucheza na Yanga. Tunataka kuitoa kwenye Ligi ya Mabingwa ili tusonge mbele,” alisema Arsene na kuongeza;

“Tuna timu bora na yenye ushindani. Tunatambua ubora wa Yanga lakini tunataka kuionyesha Afrika umahiri wetu kwa kuiondosha Yanga. Mashabiki watarajie kuiona Vital’O ikishinda na kusonga mbeleĀ  kwenye michuano hiyo.”

Vital’O leo Agosti 7,2024 imeanza safari ya kuja nchini Tanzania ambako itafikia jijini Mwanza kabla ya kuingia Dar es Salaam itakakocheza mechi hizo mbili dhidi ya Yanga.

Ikiwa Mwanza itacheza mechi ya kirafiki na Pamba Agosti, 10 mwaka huu katika kilele cha tamasha la Pamba Day, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Baada ya hapo itasalia kwa siku tatu Mwanza kisha itasafiri hadi Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Yanga Agosti 17, 2024 kisha itasalia Dar es Salaam hadi itakapomaliza mechi ya marudiano, Agosti 24 mwaka huu.

Related Posts