Wakazi Ngara walia upatikanaji wa vitambulisho vya Nida, maji

Ngara. Wakazi wa Kijiji cha Kumunazi kilichopo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameeleza kero ya kutopatiwa vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), jambo linalowakwamisha kupata baadhi ya huduma muhimu.

Wakazi hao wameeleza hayo leo Jumatano Agosti 7, 2024 mbele ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi aliposimama kuwasalimia akitokea Wilaya ya Biharamulo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro amesema moja ya changamoto wanayokutana nayo wakazi wa Kumunazi ni kukosa vitambulisho vya Taifa kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

“Wananchi wanakosa vitambulisho vya Nida, imefikiwa mahali watu wanaazima vitambulisho vya ndugu zao kwa ajili ya kusajilia laini za simu. Hii imekuwa kero kubwa kwa wananchi hawa.

“Ombi letu kwako, ni kuwasukuma hawa Nida na Uhamiaji waweze kutoa vitambulisho hivyo ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu,” amesema mbunge huyo huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza.

Mbunge huyo ameeleza pia kuna changamoto ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho na wamefanya jitihada ya kupata kibali cha kutafuta mkandarasi ili aanze kutekeleza mradi huo, lakini kibali hicho hakijatokewa hadi sasa.

“Ndugu katibu mkuu, wananchi hawa hawajawahi kupata maji tangu uhuru, tumefanya jitihada mbalimbali za kupata kibali lakini miaka miwili sasa hatujafanikiwa, tunaomba utusaidie katika hili,” amesema Ruhoro.

Akipigilia msumari kuhusu changamoto ya maji, diwani wa Kasulo, Yusufu Katula amesema wananchi wake wamekuwa wakitumia maji yasiyo safi na salama, jambo linalowasababishia magonjwa ya kuhara.

Ruhoro amebainisha pia changamoto ya kukosekana kwa umeme katika vijiji mbalimbali katika jimbo lake.

Amesema umeme umefikishwa vijijini lakini umeishia kwenye transfoma, haujawafikia wananchi majumbani, shuleni au kwenye zahanati.

Akijibu changamoto zilizoibuliwa na mbunge huyo, akianzia ile ya vitambulisho vya Nida, Dk Nchimbi amelichukua na atawaelekeza Wizara ya Mambo ya Ndani kulishughulikia ili wananchi wasikwame kupata huduma.

“Hili la vitambulisho vya Taifa tumelichukua, tutaielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani kulishughulikia. Watu kutumia vitambulisho vya watu wengine, ni kuchochea uhalifu, mtu anaweza akafanya tukio huko, wakafuatilia laini ya simu, wakakuta ni mtu mwingine. Tutalisimamia hili kuhakikisha linafanyiwa kazi.

Kuhusu changamoto ya maji, Dk Nchimbi amempigia simu Waziri wa Maji, Juma Aweso na kumuuliza kuhusu suala hilo, amemhakikishia kwamba atakwenda yeye mwenyewe kufuatilia jambo hilo.

Katibu huyo wa CCM, amemwelekeza Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu kufuatilia suala la umeme katika jimbo hilo ili wananchi wafikishiwe umeme kwenye makazi yao.

“Waziri wa Nishati popote alipo anisikie, mkuu wa mkoa, shirikiana na waziri kuhakikisha wananchi wanapata umeme,” ameelekeza Dk Nchimbi.

Related Posts