WATUMISHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUCHUNGUZA AFYA KATIKA KAMBI YA MATIBABU YA BMH

Na. Carine Abraham Senguji, Dodoma.

Watumishi wa Umma wamehimizwa kutumia fursa hii kujitokeza kwa wingi kuchunguza afya zao katika kambi ya matibabu na uchunguzi inayofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba.

Wito huo umetolewa na Ndg. Cyrus Kapinga ambae amemuwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo.

“Kambi hii imeandaliwa kwa lengo la kuwasogezea watumishi wa umma huduma za kibingwa na ubingwa bobezi wa uchunguzi, elimu, ushauri na matibabu hivyo naomba watumishi mtumie fursa hii vizuri,” amesema Ndg. Cyrus.

Ndg. Cyrus ameendelea kwa kusema huduma hizi zinatolewa bure kabisa kwa watumishi wote watakaofika kupata huduma.

“Huduma katika kambi hii ni bure kabisa kwa wale wote watakaofika kupata huduma na kwa watakaobainika kuwa na changamoto watapata rufaa ya kwenda kuendelea na uchunguzi wa kina pamoja na matibabu katika Hospital ya Kanda Benjamin Mkapa,” amesema Ndg. Cyrus

Kwa upande wake, Prof. Abel Makubi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ameshukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutoa eneo la kufanyia kambi hii ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na kushirikiana katika kufanikisha kuwepo kwa kambi hii.

“Nashukuru sana kwa ushirikiano wenu na kutoa jengo lenu kwaajili ya kambi hii ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali haswa yale yasiyoambukiza,” amesema Prof. Makubi.

Bi. Sophia Kayombo, ambaye ni mtumishi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameshukuru BMH kwa huduma nzuri alizopatiwa na madaktari wa BMH.

“Nashukuru kwa huduma nzuri nilizopata, madaktari wapo vizuri na nilipima vipimo vyote jana na Leo nimekuja kuchukua majibu yangu, nashauri watumishi wenzangu kuja kuangalia afya ili kuwa ili kuwa na uhakika wa afya zao na kupata matibabu na ushauri wa madktari,” amesema Bi. Sophia.

Kambi hii ambayo imeanza Agosti 5, 2024 na kufikia tamati Agosti 9, 2024.

Related Posts