Dar es Salaam. Hatimaye Jeshi la Polisi limevunja ukimya kuhusu tukio la msichana kubakwa na kulawitiwa na vijana watano waliodai kutumwa na afande, likieleza kuwakamata watuhumiwa wanne kati ya sita waliopanga na kutekeleza uhalifu huo.
Ukamataji huo umewagusa pia watu wengine wanane, kati yao wakiwemo wanne waliokamatwa kwa kukiuka sheria na kusambaza picha mjongeo (video) za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, zilizoonyesha tukio hilo la ukatili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi video hiyo ilianza kusambaa Agosti 2, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti msichana mmoja wakidai kuagizwa na afande.
Katika taarifa iliyotolewa Agosti 9, 2024, Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime amesema hadi sasa uchunguzi umewezesha kubaini kuwa, tukio hilo lilifanyika Mei 2024 katika eneo la Swaswa jijini Dodoma.
Amewataja waliokamatwa kwa kosa la kumlawiti na kumbaka binti huyo ni Clinton Damas jina maarufu Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.
Misime amesema watuhumiwa hao walikamatwa mkoani Dodoma na Mkoa wa Pwani, huku Jeshi hilo likiendelea kuwatafuta watuhumiwa wawili ambao hawajapatikana hadi sasa.
“Uchunguzi unaendelea kukamilishwa sambamba na kuwasaka watuhumiwa wawili ambao bado wamejificha ili wafikishwe mahakamani. Kwa hawa ambao bado wamejificha kama kuna yeyote anayefahamu wamejificha wapi atoe taarifa na asipofanya hivyo wakikamatwa wakiwa nyumbani au kwenye makazi yake atakamatwa na kufikishwa mahakamani,” amesema Misime.
Mbali na taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Misime amesema Jeshi hilo limempata binti aliyefanyiwa ukatili huo na amehifadhiwa eneo salama akiendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo.
Shauku ya wengi ilikuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa mkuu wa tukio hilo ambaye inasadikika ndiye aliyewatuma vijana hao kufanya ukatili huo.
Katika video hiyo walisikika vijana wakieleza kuagizwa kufanya kitendo hicho kama adhabu kwa msichana kwa kosa la kutembea na mume wa afande aliyewatuma.
Hata hivyo, taarifa ya Polisi ya kukamatwa kwa watu wanne waliohusika moja kwa moja katika tukio hilo ambao wote ni wanaume ni wazi kuwa bado mtuhumiwa mkuu ambaye ndiye aliyewatuma vijana hao bado hajakamatwa.
Tangu kusambaa kwa video hiyo kumekuwapo na msukumo kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali zikilitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika wa ukatili huo ili sheria ifuate mkondo wake.
Agosti 5, 2024 rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi alilitaka Jeshi la Polisi lichukue hatua stahiki za kisheria na kuhakikisha wahalifu wote waliotenda kitendo hicho na waliowezesha wakamatwe na kufikishwa mahakamani, ili haki itendeke.
Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi kupitia taarifa iliyotolewa na shirika hilo alisema, “sisi kama wadau wa haki za binadamu tunatafsiri kitendo hiki kama cha mauaji na tunatoa rai kwa Jeshi la Polisi kutumia mikakati yote ya kuwachukulia hatua stahiki wahusika wote, pia tunakemea vikali kuendelea kusambazwa kwa video hizi.”
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia kwa Mkurugenzi wake, Anna Henga kilitaka wahusika wote watano na aliyewatuma kulingana na maelezo wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Mbali na viongozi hao wa taasisi, Agosti 5 kupitia mtandao wa X watu mbalimbali walionyesha utambulisho wa vijana hao ikidaiwa baadhi yao ni wanajeshi wakilitaka Jeshi la Polisi kuwafikia na kuwakamata ili sheria ifuate mkondo wake.
Katika kushinikiza sheria ichukue hatua, wakili Peter Madeleka alisema atalazimika kuingilia kati suala hilo kama Mkurugenzi wa Mashtaka hatachukua hatua ndani ya saa 24.
“Nataka nimwambie DPP ikiwa ndani ya saa 24 kuanzia sasa atashindwa kuwapeleka mahakamani hawa mashetani kwa kisingizio chochote. Mimi Peter Madeleka nitafanya wajibu huo kwa fedha zangu. Hatuwezi kuwa na taifa la kulinda wahalifu.
“Nitakwenda mahakamani ili kuiomba mahakama iwalazimishe polisi na taasisi nyingine zitimize wajibu wao haki ya mwanamke aliyebakwa na kulawitiwa ipatikane haraka iwezekanavyo,” alindika Madeleka.
Taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha ukamataji haukuishia kwa watuhumiwa waliohusika na tukio hilo pekee bali pia waliosambaza video zilizoonyesha tukio hilo na waliosambaza taarifa za uongo.
Misime amewataja waliokamatwa kwa kosa la kusambaza video hiyo ni Frora Mlombola, Aghatha Mchome, Madatha Budodi na James Paulo ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Amesema watuhumiwa wengine wanne walikamatwa kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza taarifa za uongo mitandaoni zilizoeleza kuwa binti huyo amefariki dunia.
“Kuna waliotengeza na kusambaza taarifa za uongo zinazosema RIP. Binti aliyebakwa na kulawitiwa akutwa amefariki. Taarifa nyingine ya uongo inasema mama wa binti huyo amedondoka na kufariki,” amesema.
Amesema watuhumiwa hao wawili walikamatwa Arusha na wengine wawili walikamatwa mkoani Dar es Salaam ambao majina yao ni Amos Lwiza, Adam Dongo, Venance Mallya na Isack Elias.
Misime ameonya watu ambao hawana mamlaka ya kufanya hivyo waache tabia ya kwenda kwenye eneo ambalo lilitajwa kuwa huyo binti anaishi wakimtafuta yeye na familia yake ili wawahoji au kuwaona.
Amesema kufanya vitendo vya aina hiyo ni kuwatweza utu wao na kuwatonesha majeraha waliyonayo mioyoni mwao.
Agosti 8, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alilieleza Mwananchi kwa njia ya simu kuwa kitendo alichofanyiwa binti huyo Serikali inalaani kwa nguvu zote kwani ni kinyume cha sheria za nchi na utamaduni wa Mtanzania.
“Binti yupo mikono salama hajafa, mimi mkuu wa mkoa nafahamu kabisa yupo salama, yupo kwenye moja ya vituo vyetu na lazima binti huyo awe salama apone kisaikolojia, aweze kutulizwa vizuri na kupewa elimu ya unasihi itakayomsaidia kujikuza katika maisha yake ya kila siku,” alisema Chalamila.