ALIYEKUWA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU, AFARIKI AKIWA NA MIAKA 77 – MWANAHARAKATI MZALENDO

Issa Hayatou, aliyewahi kuwa rais wa muda mrefu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. Hayatou, raia wa Cameroon, alihudumu kwa miaka 29 kama kiongozi wa shirikisho hilo linalosimamia soka barani Afrika, akishikilia nafasi ya urais kuanzia mwaka 1988 hadi 2017.

Mbali na uongozi wake CAF, Hayatou pia alishika nyadhifa za juu katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), akiwa mjumbe wa kamati kuu ya FIFA, sasa inajulikana kama Baraza la FIFA, kuanzia mwaka 1990 hadi 2017. Katika kipindi hicho, alihudumu kama kaimu rais wa FIFA kwa muda mfupi kati ya mwaka 2015 na 2016, baada ya Sepp Blatter kusimamishwa kazi.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alitoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Hayatou kupitia chapisho kwenye Instagram, akimtaja Hayatou kama shabiki wa michezo ambaye alijitolea maisha yake katika usimamizi wa michezo. “Imenisikitisha kusikia kifo cha aliyekuwa rais wa CAF, kaimu rais wa FIFA, makamu wa rais wa FIFA, na mjumbe wa Baraza la FIFA, Issa Hayatou,” aliandika Infantino. “Kwa niaba ya FIFA, rambirambi ziende kwa familia yake, marafiki, wafanyakazi wenzake wa zamani, na wote wanaomfahamu. Pumzika kwa amani.”

Katika ujana wake, Hayatou alikuwa mwanariadha wa mbio na mchezaji wa mpira wa vikapu, kabla ya kujitosa katika usimamizi wa michezo.

Hata hivyo, Hayatou alipigwa marufuku ya mwaka mmoja mnamo Agosti 2021 kwa kukiuka kanuni za maadili za FIFA wakati wa kusaini mkataba mkubwa wa matangazo barani Afrika na kampuni ya habari ya Ufaransa ya Lagardère mwaka 2016. Adhabu hiyo ilibatilishwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo mnamo Februari mwaka uliofuata.

Kifo cha Hayatou kimeacha pengo kubwa katika historia ya soka la Afrika, akiwa mmoja wa viongozi walioleta mabadiliko makubwa katika mchezo huo barani na duniani kote.

 

#KoncptTvUpdates

#bbcnewsswahili

Related Posts