Changamoto za wadau wa usafiri majini kutatuliwa

Serikali imesema changamoto zinazowakabili wadau wa Bandari Kavu na Mawakala wa meli nchini zitatuliwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri na kuchangia kuinua mapato ya Serikali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb) leo tarehe 07 Agosti, 2024, jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kutembelea bandari kavu pamoja na wakala wa huduma za meli ili kujionea mnyororo wa sekta ya uchukuzi unavyofanya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari na wadau hao Mhe. Kihenzile amesema wadau wa sekta binafsi nchini wanasaidia kuongeza pato la Serikali kwa kulipa kodi, kutoa ajira kwa Watanzania, pamoja na kusaidia bandari kupata mzigo kwa wingi na kuondosha msongamano wa mizigo bandarini.

Amesema Serikali ingependa kuona wadau wanafanya kazi kwa kujiamini ili kuweza kuongeza mapato ya Serikali.

“Ni mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuona wadau hawa wanafanya kazi kwa kujiamini na katika mazingira ya rafiki,” amesema.

Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, wadau hao walizitaja changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa barabara za kuingia kwenye bandari kavu na muda mfupi wa leseni ambapo kanuni zinaelekeza muda wa leseni kuwa mwaka mmoja.

Bw. Bosco Haule, Meneja wa Oparesheni wa Bandari Kavu ya Bravo amesema, ubovu wa barabara ya kuingia bandarini hapo kunaleta shida hasa kipindi cha mvua ambapo maji ukwamisha shughuli nyingi.

Naye, Bw. Mbonea Bohela, Meneja Mkuu wa Bandari Kavu ya AMI amesema muda mfupi wa leseni ukatisha tamaa wawekezaji na kuiomba Serikali kuongeza muda angalau kufikia miaka mitano ili kuchagiza uwekezaji mkubwa katika biashara zao.

Kwa upande wa mawakala wa meli wameiomba Serikali iendelee kuboresha Bandari ya Dar es Salaam hasa kwenye maeneo ya mlango ili kuwezesha meli nyingi zaidi kuweza kugeuza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nelson Mlali amesema TASAC inaendelea kusimamia kwa weledi sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Serikali ili kuweza kuwahudumia wadau vizuri.

 

Related Posts