Hili hapa suluhisho migogoro ya ardhi Zanzibar

Unguja. Migogoro ya ardhi ya muda mrefu Zanzibar, huenda sasa ikapata suluhisho baada ya kuanzishwa mradi wa mfumo wa usimamizi na usajili wa ardhi (Laris).

Zanzibar yenye eneo la ukubwa wa mita za mraba 200,654, ardhi iliyopimwa ni asilimia 10 pekee.

Kutokana na hali hiyo Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imesaini mkataba wa miaka minne na Kampuni ya IGNFI kutoka nchini Ufaransa kupima ardhi kwa gharama ya mkopo wa Euro 43.1 milioni (Sh127 bilioni).

Fedha hizo ni kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI) kwa asilimia 85 na Benki ya CRDB kwa asilimia 15.

Mradi huo unaeleza kuwa na faida lukuki za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Akizungumza wakati wa utiaji saini, leo Agosti 9, 2024 Waziri wa Ardhi, Rahma Kassim Ali ametaja faida zitakazopatikana za kiuchumi na kijamii kuwa ni kupunguza migogoro, hivyo kuongeza amani na usalama katika jamii.

“Kupanga miji bora kunaweza kuboresha maisha ya watu kwa kuwa na miundombinu bora na huduma za kijamii, na kuongeza pato la Taifa kwa kuongeza idadi ya miamala ya ardhi. Pia kuwezesha ukusanyaji wa kodi za majengo kwa ufanisi,” amesema.

Jambo lingine linalotajwa kutokana na mradi huo ni kuongeza ufanisi wa matumizi ya ardhi na kuchochea shughuli za kiuchumi, kuimarisha uwekezaji nchini na kuweka mazingira bora ya kukuza utalii.

Katika hatua hiyo, amesema wananchi watapata uhakika wa umiliki wa ardhi, kupata mikopo, kuongeza uzalishaji na mapato.

Kwa upande wa kisiasa mfumo huo unatajwa kuongeza utulivu kwa kuzuia migogoro ya ardhi kuwa chanzo cha mivutano na migongano ya ardhi katika jamii, na kuimarisha taasisi za kisheria hususani zinazosimamia sekta ya ardhi na kusaidia kujenga Serikali imara na yenye ufanisi.

Pia, utasaida kuimarisha na kusimamia sera nzuri za ardhi kwa lengo la kuboresha au usimamizi wa miji na kuimarisha uongozi wa kisiasa kwenye ngazi za shehia na kitaifa, huku utawala wa sheria nao ukiimarishwa ambao utaongeza imani ya wananchi kukuza uchumi.

Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo ametaja maeneo makuu manane ambayo yatafanyika ndani ya mradi huo ikiwa ni pamoja na Kituo cha Taarifa za Ardhi (ZLIC) na vituo vya huduma vya kimkoa.

Mengine ni ubadilishaji wa nyaraka za ardhi kidijitali na mfumo jumuishi wa taarifa za ardhi na usimamizi wa mabadiliko na kuwajengea uwezo watendaji, utambuzi na usajili wa ardhi.

Mfumo huo wa Laris unalenga kuunganisha kidijitali taarifa za ardhi kuhusu umiliki, upimaji, mipango miji, uthamini, usajili na matumizi mengine ya ardhi na bahari ndani ya mipaka ya Zanzibar.

“Laris utakuwa mfumo imara utakaounganisha taarifa hizo zote zilizosambaa katika taasisi mbalimbali za umma na kusababisha ugumu na ucheleweshaji katika kutataua migogoro ya ardhi Zanzibar,” amesema.

Meneja Mkuu wa IGNFI, Christopher Dekeyne amesema mradi huo utakuwa ukienda sambamba na shughuli tofauti za miundombinu ya data ya anga, mpango mkuu na ujenzi wa majengo.

Amesema shughuli hizo za kiufundi zinafanywa kwa njia ya uhamisho wa teknolojia na kujenga uwezo kwani wanataka Wizara ya Ardhi ndiyo iwe mmiliki wa yote hayo.

“Ili kuendesha mradi huo na kuhakikisha mafanikio, IGNFI imekusanya rasilimali zake yenyewe washirika waliofanyiwa majaribio bora kwenye baadhi ya maeneo mahususi,” amesema.

“Ni fahari kubwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesadikishwa na mbinu yetu, na kuamini uzoefu wa kipekee wa IGNFI, tunaahidi kuheshimu uaminifu huo,” amesema.

Related Posts