Mwanasiasa huyo amesema yuko tayari kuachana na chama hicho wakati wowote iwapo ataona kimeacha misingi iliyomsukuma kujiunga nacho.
Lissu ambaye ni mwanasiasa mwenye udhubutu amesema chama hicho siyo mama yake akijaribu kunukuu kauli ambayo pia imewahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyekuwa akizungumzia ukaribu wake na chama tawala CCM baada ya kung’atuka katika siasa.
Msigwa awakosoa viongozi wa Chadema
Bila kubainisha bayana, Lissu amesema hatakawi kukipa mkonowa kwaheri chama chake hicho na atafanya hivyo pale atakapoona mwenendo wa Chadema siyo ule tena uliomsukuma kujiunga nao yapata miaka iliyopita.
Matamshi yake yanakuja huku aliyekuwa mmoja wa vigogo wake, Peter Msigwa aliyejiunga na chama tawala CCM katika miezi ya hivi karibuni akiendelea kuzunguka katika majukwaa na kuwakosoa baadhi ya viongozi wa chadema na sera zake.
Msigwa ambaye katika siku zake za mwisho mwisho ndani ya Chadema alikuwa akizunguka katika mikutano ya kisiasa na Lissu amekuwa akimlenga zaidi, mwenyekiti Freeman Mbowe akimtuhumu kwa mambo mbalimbali.
Kauli ya Lissu imezua mjadala mkubwa huku wengine wakidadisina kushindwa kutoa majibu ya moja kwa moja hasa kutokana na uzito wa kiongozi huyo katika siasa za vyama vya upinzani.
Fukuto ndani ya chama cha upinzani
Jambo linalowasukuma wachambuzi wa mambo kudadisi kauli yake hiyo ni hasa wakati huu ambako sehemu kubwa ya vyama vyenye usajili rasmi vimekuwa katika hatua ya kupanga mikakati ya kujiimarisha kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.
Katika tathmini yake juu ya kauli hiyo, mtaalamu wa masuala ya siasa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt Richard Mbunda anasema huenda kuna fukuto linaloendelea ndani ya chama hicho.
Haijajulikana mara moja kama matamshi hayo ya Lissu yalichomoza wakati wa kikao cha kamati kuu ya Chadema ambacho kimekuwa kikikutana jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali ikiwemo yale yanayohusu uchaguzi wa serikali za mitaa.