Jeshi la Israel lashambulia shule Gaza na kuwaua watu 18 – DW – 09.08.2024

Afisa wa ngazi ya juu wa shirika hilo, Mohammad al-Mughayyir amesema shambulizi la Israel lilitokea Alhamisi katika shule za Al-Zahra na Abdel Fattah Hamoud mjini Gaza.

Mughayyir amesema watu 60 walijeruhiwa na zaidi ya wengine 40 bado hawajulikani walipo. Amesema ni wazi kuwa Israel ilizilenga shule hizo na maeneo salama ya kiraia katika Ukanda wa Gaza.

Jeshi ladai shule zinatumika na magaidi

Hata hivyo, jeshi la Israel limesema shule hizo zilikuwa na vituo vya kamandi vya Hamas. Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa maeneo ya shule yalikuwa yanatumiwa na magaidi na makamanda wa Hamas, ambapo walipanga na kufanya mashambulizi.

Kwengineko huko Gaza, watu wapatao 13 waliuawa. Duru za afya na waokoaji wamesema hayo, wakati ambapo jeshi la Israel likitoa amri mpya ya watu kuondoka kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa kusini wa Khan Yunis.

Wapalestina wakiwa katika mji wa Khan Yunis
Wapalestina wakiwa katika mji wa Khan Yunis Picha: Hatem Khaled/REUTERS/REUTERS

Mohammed Abdeen, mkaazi wa Khan Yunis anasema yeye pamoja na mamia ya Wapalestina wasio na makaazi wameanza kuondoka katika eneo hilo, baada ya amri hiyo kutolewa.

“Tumehamishwa mara 15, hii inatosha. Sisi ni raia na hatupaswi kulaumiwa kwa hili. Vita vyenu mnapigana na Hamas, na sio sisi. Sisi ni watu, sisi ni raia, kwa nini tunahusishwa? ” Aliuliza Abdeen.

Tayari jeshi la Israel limeanzisha operesheni mpya za kijeshi huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Israel yakubali kurejea kwenye meza ya mazungumzo

Ama kwa upande mwingine, Israel imekubali kurejea kwenye meza ya mazungumzo ikiwa ni katika kutafuta usitishwaji wa mapigano Gaza yaliyopangwa kufanyika Agosti 15, kwa maombi ya wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri. Taarifa hiyo ilitolewa Alhamisi na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huku mvutano wa kikanda ukiongezeka na kuwepo wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzuka vita kamili.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana, viongozi wa nchi hizo tatu wamezialika pande zinazohasimiana kurejea katika meza ya mazungumzo mjini Doha au Cairo, ili kuziba mapengo yote yaliyosalia na kuanza utekelezaji wa makubaliano bila kuchelewa zaidi.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali BagheriPicha: Hadrien Dure/BELGA/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, Iran imeituhumu Israel kutaka kueneza vita katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa Israel imefanya kosa kubwa la kimkakati kumuuwa kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh mjini Tehran, wiki iliyopita, saa chache baada ya kuuwawa kwa mkuu wa kijeshi wa kundi la Hezbollah mjini Beirut.

Ingawa Israel haijakiri kumuua Haniyeh, Iran na washirika wake wameapa kulipiza kisasi, huku vita vya Gaza vikiingia mwezi wake wa 11. Bagheri amesema Israel inataka kuutanua mzozo, vita na migororo hadi nchi nyingine, lakini haina uwezo wala nguvu ya kupambana na Iran.

 

(AFP, DPA, Reuters)

Related Posts